Habarika | WAWAKILISHI 'SABA' WA TANZANIA KWENYE MICHUANO YA OLIMPIKI WATAKIWA KURUDI 'MEDALI'
layout-wrap boxed
Friday, April 27, 2018

WAWAKILISHI ‘SABA’ WA TANZANIA KWENYE MICHUANO YA OLIMPIKI WATAKIWA KURUDI ‘MEDALI’

Serikali imeitaka timu ya Tanzania itakayoshiriki Michezo ya 31 ya Olimpiki kuhakikisha inarejea na medali kutoka katika michezo hiyo nchini Brazil.

Michezo hiyo itaanza Ijumaa ya wiki hii hadi Agosti 21 ambapo timu hiyo yenye wachezaji wa riadha (4), kuogelea (2) na judo (1), iliagwa jana na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura kwenye Uwanja wa Taifa.

Wambura katika hafla hiyo alisema kuwa anatambua changamoto walizopitia wanamichezo hao wakati wa maandalizi ya kushiriki michezo hiyo mikubwa inayoshirikisha zaidi ya mchezo mmoja duniani.

Pia, naibu waziri huyo aliwapongeza wanamichezo wote waliofuzu na wale wanaoshiriki michezo hiyo kwa nafasi za upendeleo kwa jitihada zao walizofanya wakati wakijiandaa kwa michezo hiyo.

Aliwataka wachezaji hao kupambana ili kupeperusha vizuri bendera ya Tanzania na kutangaza utamaduni wa Tanzania zikiwemo ngoma za asili. Pia aliwapongeza wadhamini mbalimbali, ambapo aliwataka kudhamini na michezo mingine ambayo haipewi kipaumbele.

Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Elisante ole Gabriel aliwataka Bodi ya Utalii (TTB) kuwapeleka wanamichezo hao katika mbuga za wanyama watakaporejea kutoka Brazil.

Wanariadha wanaounda timu hiyo ni Alphonce Felix, Said Makula, Fabian Joseph na mwanadada pekee katika riadha, Sarah Ramadhani, ambao wote watashiriki marathon.

Waogeleaji ni Magdalena Moshi na Hilal Hemed Hilal wakati mchezaji pekee wa judo ni Andrew Thomas. Makocha watakaoongozana na timu hizo ni Francis John (riadha), Alexander Mwaipasi (kuogelea) na Zaid Hamisi (judo) wakati daktari wa timu ni Nassoro Matuzya.

Waogeleaji na mchezaji huyo wa judo na makocha wao wanaoondoka leo kwa ndege mbili tofauti huku mwanariadha wakike ataondoka Agosti 10 na wale wakiume wataondoka Agosti 15. Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi alisema timu hiyo inaondoka kwa awamu kutokana na ratiba za ndege.

Timu ya judo itaondoka kwa ndege ya Afrika Kusini na kundi la pili litakuwa la kuogelea, ambalo litaondoka saa tisa alasiri na Emirates. Nahodha wa timu hiyo Felix alisema timu ya riadha imejiandaa vizuri baada ya kufanya mazoezi kwa muda mrefu, ambapo aliahidi kurudi na medali.

Sambaza Makala hii: Share on Facebook1Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn0Share on Google+0Email this to someone

You may also like

0 comments

By