Habarika | RIPOTI: WATOTO MILIONI 69 WA CHINI YA MIAKA MITANO KUPOTEZA MAISHA KWA MAGONJWA IFIKAPO MWAKA 2030
layout-wrap boxed
Tuesday, May 22, 2018

RIPOTI: WATOTO MILIONI 69 WA CHINI YA MIAKA MITANO KUPOTEZA MAISHA KWA MAGONJWA IFIKAPO MWAKA 2030

Watoto milioni 69 walio na umri wa chini ya miaka mitano duniani watapoteza maisha kwa magonjwa yanayoweza kuzuilika, watoto milioni 167 wataishi kwenye dimbwi la umasikini huku watoto wengine milioni 750 wako hatarini kuolewa wakiwa na umri wa utoto ifikapo mwaka 2030, imeelezwa.

Ripoti ya mwaka ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) imeeleza hatari hiyo kwa watoto inatokana na serikali za nchi zao, nchi wahisani na jumuiya za kimataifa kutokuweka juhudi na mipango yoyote ya kushughulikia tatizo hilo.

“Kushindwa kuwajali mamilioni ya watoto hawa ili waweze kuwa na maisha mazuri sio athari kwa watoto hao peke yake, bali ni hasara ambayo jamii yote itaishuhudia kwa siku za mbele,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Unicef, Anthony Lake na kuongeza; “Tuna uchaguzi wa kufanya, kuwekeza kwa watoto hao sasa au turuhusu dunia inayokuja iwe na matabaka ya kijamii pasipo usawa.”

Ripoti hiyo iliyotolewa jana New York, Marekani imesema kuna haja ya kuweka mikakati itakayosaidia watoto waende shule pamoja na kuwainua ili waondoke kwenye dimbwi la umasikini.

Alisema takwimu za dunia zinaonesha kuwa vifo vya watoto wa chini ya miaka mitano vinaongezeka kuliko ilivyokuwa miaka ya 1990, wavulana na wasichana wanakwenda shule kwa usawa katika nchi 129, lakini watu katika nchi hizo wanaishi katika umasikini wa hali ya juu, idadi inayokadiriwa kuwa nusu ya ile ya miaka ya 1990.

Ripoti hiyo imeeleza watoto ambao ni masikini zaidi idadi yao imeongezeka mara mbili zaidi na wako hatarini kupoteza maisha kabla ya kufikisha miaka mitano.

Maeneo ya kusini mwa Bara la Asia na Kusini mwa Jangwa la Sahara, idadi ya watoto wanaozaliwa na mama zao ambao hawana elimu idadi imeongezeka mara tatu na wako hatarini pia kupoteza maisha wakiwa chini ya umri wa miaka mitano kuliko wale ambao wanazaliwa na mama ambao wana elimu walau ya sekondari.

Wasichana ambao wanatoka kwenye kaya masikini zaidi nao wameongezeka mara mbili kuliko idadi ya wasichana ambao wanazaliwa kwenye familia zenye kipato cha kati.

Hali ni mbaya zaidi katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambako ripoti hiyo imefafanua kuwa walau watoto milioni 247 wanaishi kwenye umasikini mkubwa. Inaelezwa kuwa asilimia 60 ya watu wenye umri kati ya miaka 20 na 24 kutoka kaya masikini wamepata elimu ya msingi chini ya miaka minne.

Sambaza Makala hii: Share on Facebook2Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn0Share on Google+0Email this to someone

You may also like

0 comments

By