Habarika | VITA YA MAGUFULI DHIDI YA RUSHWA NA UFISADI YAITIA MOYO CHINA
layout-wrap boxed
Tuesday, May 22, 2018

VITA YA MAGUFULI DHIDI YA RUSHWA NA UFISADI YAITIA MOYO CHINA

Chama cha Kikomunisti cha Watu wa China (CPC) kimesema uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, umeonesha nia ya dhati katika kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi.

Aidha, CPC imesema Rais Magufuli ameonesha nia ya kuinua hali za maisha ya Watanzania na kuinua uchumi wa taifa kwa ujumla na kutaka juhudi hizo kuungwa mkono na Watanzania wote ili kuhakikisha maendeleo ya kweli yanapatikana kwa wananchi.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa China na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CPC, Guo Yezhou alitoa kauli hiyo jana mjini hapa mara baada ya ziara yake mkoani Dodoma. Guo alisema Rais Magufuli ni kiongozi aliyeonesha nia ya kupambana na rushwa, kuinua uchumi wa taifa na kuinua hali ya maisha ya Watanzania.

“China na CPC wataendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ambazo ni kuhakikisha taifa linapiga hatua zaidi za kimaendeleo na kutokomeza umaskini,” alisema Naibu Waziri huyo. Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa alisema CCM inajivunia urafiki wake na nchi ya China ambao ni wa muda mrefu.

“CCM inathamini urafiki na udugu huo,” alisema Kimbisa. Ujumbe huo kutoka Chama cha Kikomunisti cha China pia ulikutana na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Phillip Mangula na kuzungumzia masuala mbalimbali ya uhusiano na ushirikiano baina ya vyama hivyo viwili.

Aidha, ujumbe huo ulipokuwa mkoani Dodoma ulipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ikiwemo Ofisi za CCM Mkoa wa Dodoma, hosteli zinazomilikiwa na CCM, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Ukumbi mpya wa Mikutano wa CCM na Uwanja wa Michezo wa Jamhuri unaomilikiwa na CCM.

Pia Naibu Waziri huyo wa China alikabidhiwa zawadi mbalimbali za wenyeji wake, ikiwemo kinyago kilichochongwa kwa kutumia mti wa mpingo na vazi la asili la kabila la Kigogo maarufu kama mgolole.

Alisema hiyo itakuwa kumbukumbu nzuri sana kwake na zawadi hizo ni kielelezo tosha cha upendo walionao Watanzania. “Nikiwa na vazi hili naweza kuingia nchini bila viza,” alisema Waziri huyo akimaanisha vazi kama hilo ni utambulisho halisi wa Mtanzania.

Sambaza Makala hii: Share on Facebook2Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn0Share on Google+0Email this to someone

You may also like

0 comments

By