Habarika | VIKUNDI VYA WAKULIMA KUNUFAISHWA NA SH BILIONI 40 ZA BENKI YA KILIMO
layout-wrap boxed
Sunday, February 25, 2018

VIKUNDI VYA WAKULIMA KUNUFAISHWA NA SH BILIONI 40 ZA BENKI YA KILIMO

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) itatumia zaidi ya Sh bilioni 40 kutekeleza mpango wa pili wa maendeleo wa taifa kwa kuvipa mikopo vikundi vya wakulima nchini. Mpango huo wa miaka mitano utaanza kutekelezwa mwaka 2016/17 hadi 2020/21.

Umejikita kuhakikisha Tanzania inajenga uchumi wa viwanda na kuongeza kiwango cha ajira na uzalishaji. Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Thomas Samkyi aliyasema hayo wakati akizungumza na wanahabari Dar es Salaam jana.

Alisema, benki hiyo imeamua kusaidia utekelezaji huo ili kuwezesha upatikanaji wa utoshelezi na usalama wa chakula ambao ni endelevu nchini. Pia, alisema umenuia kuleta mapinduzi ya kilimo kutoka kwenye cha kujikimu kuwa cha kibiashara, hivyo kuchangia kukuza uchumi na kupunguza umasikini.

“Ili kuhakikisha tunaunga mkono sera ya kujenga uchumi wa viwanda nchini, benki ya kilimo itatoa mikopo ya zaidi ya Sh bilioni 40 kwa wakulima. Itakuwa ni ya muda mfupi, wa kati na mrefu, kwa riba nafuu ya kati ya asilimia saba hadi 12 kwa mwaka,” alisema Semkyi.

Alisema mikopo hiyo inalenga kuwanufaisha wakulima wadogo, wa kati na wakubwa kwa ajili ya kuziba pengo la upatikanaji wa fedha za kwenye mnyororo wa ongezeko la thamani katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na mazao ya misitu.

Pia TADB itasaidia upatikanaji wa malighafi kwa viwanda vya ndani hivyo kusukuma ndoto ya serikali kufikia lengo lake la kujenga uchumi wa viwanda. Benki hiyo pia imelenga kuongoza katika utoaji mikopo kwa viwanda vidogo na vyakati vya usindikaji na uchakataji mazao ya kilimo na mifugo katika kuyaongezea thamani kwenye shughuli za kilimo.

Pia, alisema benki hiyo tangu kuanzishwa imetoa elimu kwa wakulima na kuwawezesha kupata mikopo kupitia vikundi vya ushirika 89 vilivyopatiwa elimu mkoani Iringa, vyenye wakulima 21,526.

Upande wa mikopo kwa wakulima ilishatoa mikopo kwa vikundi nane vya wakulima 857 na sasa inashughulikia maombi ya mikopo kwa awamu nyingine yenye thamani hiyo. Mkurugenzi wa Mikopo na Usimamizi wa Biashara wa Benki hiyo, Robert Pascal alisema, kwa miradi mikubwa ya kilimo inayoendeshwa kati ya serikali, taasisi za serikali na sekta binafsi, mikopo ya moja kwa moja itatolewa kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya kilimo hasa kuimarisha mifumo ya minyororo ya kuongeza thamani katika mazao.

Pascal alieleza kuwa benki hiyo itatumia bidhaa mbalimbali zenye ubunifu katika kuwezesha vikundi vya wakulima wadogo, wafugaji wa ng’ombe, samaki na kuku. Aidha, alisema benki hiyo inatarajia kuwafikia Watanzania wengi zaidi hasa vijana wanaojishughulisha na kazi za kilimo kwa kuwapatia mikopo lakini kupitia vikundi.

Alisema TADB inataraji kuvifikia vikundi zaidi ya 100,000 ambavyo katika kila kikundi kinaundwa na wanachama takribani 100, hivyo wanataraji kutoa mchango mkubwa zaidi katika sekta ya kilimo hasa kupitia kundi la vijana.

Sambaza Makala hii: Share on Facebook0Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn0Share on Google+0Email this to someone

You may also like


Warning: file_get_contents(http://graph.facebook.com/?ids=http://habarika.com/vikundi-vya-wakulima-kunufaishwa-na-sh-bilioni-40-za-benki-ya-kilimo/): failed to open stream: HTTP request failed! HTTP/1.1 403 Forbidden in /home/habarika/public_html/wp-content/themes/habarika/elements/element.php on line 80
0 comments

By