Habarika | KUMEKUCHA KISUTU: VIGOGO WA BANDARI WAKUTWA NA KESI YA KUJIBU
layout-wrap boxed
Tuesday, May 22, 2018

KUMEKUCHA KISUTU: VIGOGO WA BANDARI WAKUTWA NA KESI YA KUJIBU

Vigogo wawili wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), wanaokabiliwa na mashitaka ya matumizi mabaya ya madaraka, wamepatikana na kesi ya kujibu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Cyprian Mkeha, alisema hayo baada ya kupitia ushahidi wa upande wa Jamhuri na kuona washitakiwa wanatakiwa kujitetea.

Vigogo hao ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Ephraim Mgawe na aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Hamadi Koshuma.

Akitoa uamuzi huo, Hakimu Mkeha alisema, baada ya kupitia ushahidi wa upande wa Jamhuri ameona unajenga kesi na washtakiwa wanatakiwa kujitetea, hivyo mahakama inawaona wote wana kesi ya kujibu.

Baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, Mgawe alidai atakuwa na mashahidi tisa akiwemo yeye, na Koshuma alidai atajitea mwenyewe ambapo washtakiwa wote watatoa ushahidi wao kwa njia ya kiapo.

Washitakiwa hao wanadaiwa, Desemba 5 mwaka 2011, wakiwa watumishi wa Bandari, katika utendaji wao wakazi kwa makusudi walitumia madaraka yao vibaya kwa kusaini mkataba wa kibiashara bila kuitisha zabuni.

Mkataba huo ulikuwa baina ya TPA na Kampuni ya ujenzi ya Communication and Construction ya China (CCCC), ambao ulikuwa unahusu ujenzi wa gati namba 13 na 14 katika bandari ya Dar es Salaam, bila kuitisha zabuni.

Inadaiwa kuwa, kitendo hicho kilikuwa kinaipa manufaa Kampuni ya China. Vigogo hao wapo nje kwa dhamana ya wadhamini wawili waliosaini hati ya Sh milioni mbili kila mmoja.

Sambaza Makala hii: Share on Facebook0Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn0Share on Google+0Email this to someone

You may also like

0 comments

By