Habarika | UTAFITI: WATANZANIA MILIONI 2.3 AMBAO NI NGUVU KAZI YA TAIFA HAWANA AJIRA
layout-wrap boxed
Sunday, February 25, 2018

UTAFITI: WATANZANIA MILIONI 2.3 AMBAO NI NGUVU KAZI YA TAIFA HAWANA AJIRA

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema Watanzania milioni 2.3 kati ya watu milioni 22.3 ambao ndio nguvu kazi ya taifa hawana ajira. Kiwango hicho cha ukosefu wa ajira kwa mujibu wa NBS ni sawa na asilimia 10.3 ya nguvu kazi ya taifa. Kiwango hicho kinaelezwa kuwa kimepungua kutoka asilimia 11.7 ya mwaka 2006.

Hata hivyo utafiti huo umebainisha kuwa watu ambao hawana ajira wamebainika wanatumia muda mrefu zaidi kusaka ajira. Kwenye utafiti huo imebainishwa kuwa kiwango cha ukosefu wa ajira kwa muda mrefu kimeongezeka kutoka asilimia 17.9 mwaka 2006 hadi asilimia 32.5 mwaka 2014 huku wanawake ndio kundi kubwa la Watanzania ambao wana kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira kuliko wanaume.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi ambao ulifanyika mwaka 2014 kwa wahariri wa vyombo vya habari, Kaimu Meneja wa Takwimu za Ajira na Bei, Ruth Minja alisema idadi ya Watanzania ambao wanajihusisha katika sekta ya kilimo imepungua kutoka asilimia 73.1 hadi kufikia asilimia 66.3.

Minja alisema kiwango cha ajira katika sekta isiyo rasmi kimeongezeka karibu mara tatu kutoka asilimia 10.1 hadi kufikia asilimia 21.7 na hivyo akashauri urasimishaji wa sekta hiyo kuwa ni muhimu kwa kuwa itasaidia kuongeza tija na kuchangia kwenye kukua kwa pato la taifa.

Aliongeza kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana nacho kimepungua kidogo kutoka asilimia 13.2 hadi asilimia 11.7, lakini akatahadharisha kuwa tofauti kati ya kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana wa kike na wa kiume imezidi kuwa kubwa mwaka 2014 ikilinganishwa na mwaka 2005. Pia alisema asilimia 17.2 ya watu ambao wana uwezo wa kufanya kazi hawana kazi na wala hawako tayari kufanya kazi yoyote ya kiuchumi. Katika kundi hilo wamo wanawake ambao wengi wao wanajishughulisha na shughuli za nyumbani.

CHANZO: HABARILEO

Sambaza Makala hii: Share on Facebook4Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn0Share on Google+0Email this to someone

You may also like

0 comments

By