Habarika | SHILINGI TRILIONI 107 KUTEKELEZA MPANGO WA TAIFA WA MAENDELEO KWA MIAKA MITANO
layout-wrap boxed
Tuesday, May 22, 2018

SHILINGI TRILIONI 107 KUTEKELEZA MPANGO WA TAIFA WA MAENDELEO KWA MIAKA MITANO

Shilingi trilioni 107 zinahitajika kugharamia utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo unaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2016/21, ambao utategemea sana makusanyo ya kodi na ukijikita katika kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya viwanda.

Akiwasilisha bungeni jana Mpango huo wa Pili wa Maendeleo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango alisema katika fedha hizo, Sh trilioni 59 zitatolewa na serikali, huku kiasi kilichobaki cha Sh trilioni 48 zitachangiwa na sekta binafsi pamoja na mikopo na misaada kutoka nje.

Akitoa mchanganuo wa ugharamiaji mpango huo, Dk Mpango alisema kila mwaka serikali itatoa Sh trilioni 11.8 na kwamba katika kipindi cha miaka mitano ya mpango huo, serikali itakuwa imetoa jumla ya Sh trilioni 59.

Alisema eneo la pili la gharama za mpango huo, litabebwa na sekta binafsi, mkopo na misaada kutoka nje na kuwa serikali inaweka mazingira mazuri kwa sekta binafsi kuwekeza katika miradi ya maendeleo.

Alisema katika mpango huo, kuna ongezeko kubwa la fedha za kugharamia mpango huo, ukilinganisha na ule wa kwanza na sababu ya ongezeko hilo ni ukubwa wa miradi tarajiwa sambamba na ni ya kuchochea upatikanaji wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji wa biashara na uwekezaji.

Alisema nchi ikiwekeza kwenye ujenzi wa viwanda, huvutia misaada kutoka nje na hiyo imetokana na uzoefu wa nchi nyingine zilizoweka mikakati kwenye uwekezaji wa viwanda. “Mantiki yetu ni kwamba nchi haina budi kuwa na mkakati mahususi wa kukusanya fedha kuwezesha utekelezaji wa mpango huu kwa ufanisi,” alisema Dk Mpango.

Kwa upande wa serikali, Dk Mpango alisema fedha za kugharamia mpango huo, watazipata kwenye makusanyo ya kodi na yale yasiyo ya kodi, ambapo serikali imeainisha miradi mikubwa ya kielelezo kama ile ya makaa ya mawe ya Mchuchuma na Chuma cha Liganga.

Sambaza Makala hii: Share on Facebook1Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn0Share on Google+0Email this to someone

You may also like

0 comments

By