Habarika | SAKATA LA UFICHAJI SUKARI: MAKONDA AAMURU MOHAMED ENTERPRISES KUCHUNGUZWA
layout-wrap boxed
Saturday, March 24, 2018

SAKATA LA UFICHAJI SUKARI: MAKONDA AAMURU MOHAMED ENTERPRISES KUCHUNGUZWA

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameagiza kuchunguzwa kwa sukari kontena 115 ambayo ni zaidi ya tani 3,000 iliyokutwa katika bandari kavu ya PMM iliyopo eneo la Vingunguti.

Makonda alitoa agizo hilo jana wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika bandari hiyo na kubaini uwepo wa sukari hiyo ambayo ni mali ya Mohamed Enterprises, ambayo kwa taarifa zake aliambiwa zilikuwa kontena 165.

Alisema anazitaka mamlaka zinazohusika kama Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), pamoja na Shirika la Viwango (TBS) kuichunguza sukari hiyo kutokana na sababu mbalimbali zilizojitokeza katika uwepo wa sukari hiyo kama sukari kuagizwa kutoka Dubai lakini imetoka Brazil na imepakiwa Dubai, na upangwaji wa kontena hizo katika bandari hiyo.

“Nashindwa kuelewa kwa nini sukari iagizwe kutoka Dubai lakini itoke Brazil na kufungashwa Dubai inaonesha inaweza kuwa imeshawahi kuisha muda wake hivyo nataka ichunguzwe na tunataka tujue kama Mohamed Enterprises anaficha sukari ili ipelekwe kwa wananchi kwa matumizi,” alisema Makonda.

Mbali na kutoa maagizo hayo, Makonda pia amezuia kutumika kwa sukari mifuko 22,000 iliyokutwa katika ghala la Mohamed Enterprises Tanzania Limited (MeTL) lililopo Barabara ya Nyerere na kutaka wapeleke vielelezo kuhusu sukari hiyo kwa mamlaka zinazohusika kama ya matumizi yoyote.

Alisema sukari hiyo inayodaiwa kuwa ni ya viwandani ni lazima iangaliwe kama kweli ipo kwa ajili ya mahitaji ya viwandani au ilikuwa itumike tofauti na ilivyokusudiwa. Kwa upande wake, Meneja Operesheni wa bandari kutoka MeTL, Firoz Ebrahim alisema sukari hiyo imefuata taratibu zote na imefika katika bandari hiyo wiki moja iliyopita.

Katika hatua nyingine, Kampuni ya Al Naeem iliyopewa agizo la saa 36 kuanzia juzi iwe imeshaanza kusambaza sukari kwa bei elekezi iliyokuwa katika bandari ya Dar es Salaam, imeanza kutekeleza agizo hilo jana jioni.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Meneja wa kampuni hiyo, Haruni Zakaria alisema juzi wakati Takukuru na Polisi walipofanya ukaguzi wa sukari hiyo, walishindwa kufanikisha utaratibu wa uondoaji wa mizigo bandarini na hivyo ikawalazimu kumalizia taratibu hizo jana na jioni wakaanza kutoa sukari. Imeandikwa na Sophia Mwambe na Ikunda Erick.

Sambaza Makala hii: Share on Facebook2Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn0Share on Google+0Email this to someone

You may also like

0 comments

By