Habarika | NAIBU SPIKA AWATAKA WATANZANIA KUTOKUBALI KUPOTOSHWA NA KAMBI YA UPINZANI
layout-wrap boxed
Sunday, February 25, 2018

NAIBU SPIKA AWATAKA WATANZANIA KUTOKUBALI KUPOTOSHWA NA KAMBI YA UPINZANI

Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amewataka Watanzania wasikubali kupotoshwa na Kambi Rasmi ya Upinzani iliyoamua kususa vikao anavyoviongoza kwa kuwa kuna fursa ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi wake kama amekosea.

Akizungumza bungeni jana mchana, Dk Tulia alisema kanuni zinataka Kiti cha Spika kutumia madaraka yake kuhakikisha kanuni hazikiukwi, na kama amekosea na kwa kuwa yeye ni mwanadamu, kanuni zimetoa fursa ya kukata rufaa.

Kanuni hizo kwa mujibu wa Naibu Spika, zinataka mlalamikaji kupeleka madai yake kwa Katibu wa Bunge, ambaye atawasilisha kwa Kamati ya Kanuni na kama yanamhusu Spika, kiongozi huyo wa Bunge atatakiwa kuacha kuongoza kikao cha kamati hiyo.

Baada ya Spika kuondoka katika nafasi ya kuongoza Kamati hiyo, wajumbe wa kamati hiyo hutakiwa kumchagua mmoja wao kuwa Mwenyekiti, ambaye ataongoza kamati hiyo wakati wa kumjadili Spika hatua ambayo wabunge wanaomlalamikia, hawajaichukua.

Wakati Naibu Spika akitoa ufafanuzi huo, wabunge wa CCM wamemtaka Dk Tulia kukaza uzi na ikiwezekana aendelee kuongoza vikao vyote asubuhi na jioni, ili wabunge hao wa kambi ya upinzani waendelee kukaa nje.

Mbunge wa Mpwapwa, George Lubeleje (CCM), alisema tabia ya wabunge wa upinzani kugeuza Bunge mkutano wa hadhara, hajawahi kuiona katika vipindi vitano alivyokuwa mbunge katika Bunge hilo.

Naye Mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge (CCM) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bunge, alisema yeye hatakuwa nyuma yake, bali atakuwa bega kwa bega na Naibu Spika. Chenge alimtaka Naibu Spika na wabunge wa CCM kutojiona wanyonge kwa kuwa kinachoendelea ni mchezo wa siasa.

“Mimi Naibu Spika sipo nyuma yako, nipo bega kwa bega na wewe, hakuna haja ya kuwa na wasiwasi,” alisema Chenge. Naye Mbunge wa Uyui, Almasi Maige (CCM) alisema wanaompinga Naibu Spika hawamfahamu kuwa ni mtu mwenye msimamo tangu alikotoka kabla hata ya kuingia bungeni.

Alisema wanaodai kuwa Naibu Spika kapelekwa bungeni na Rais, Dk John Magufuli, wanapotosha kwa kuwa wabunge ndio waliomchagua katika nafasi hiyo. “Hawa hawakufahamu msimamo wako, wewe ni mpole, mtoto wa masikini uliyesoma shule za kawaida na huko ulikotoka ulitekeleza majukumu yako kwa ufanisi,” alisema Maige.

Sambaza Makala hii: Share on Facebook1Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn0Share on Google+0Email this to someone

You may also like

0 comments

By