Habarika | MRADI WA KUSAMBAZA UMEME VIJIJINI KWA AWAMU YA TATU KUNUFAISHA VIJIJI 8000
layout-wrap boxed
Sunday, April 22, 2018

MRADI WA KUSAMBAZA UMEME VIJIJINI KWA AWAMU YA TATU KUNUFAISHA VIJIJI 8000

Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, unaosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), utaanza rasmi kutekelezwa mwezi ujao, imefahamika.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo mjini Dodoma wakati akijibu hoja za wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, waliokutana na watendaji wa wizara hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo, Profesa Muhongo ameongeza kuwa katika utekelezaji wa mradi huo, serikali imepanga kuwakabidhi makandarasi watakaotekeleza mradi huo kwa wabunge ili kuhakikisha kwamba mradi husika unatekelezwa kikamilifu.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2016/17 bungeni mwaka jana, Profesa Muhongo alisema serikali itafanya tathimini ya kina ya awamu ya kwanza na ya pili ya kupeleka umeme vijijini, lengo likiwa ni kuboresha maandalizi ya utekelezaji wa awamu ya tatu ya mradi huo.

Alisema pamoja na tathimini hiyo, masuala yatakayozingatiwa katika awamu ya tatu ni kupeleka umeme kwenye vijiji ambavyo havikupata umeme katika awamu ya kwanza na ya pili; kwenye viwanda vidogo vya uzalishaji mali; na katika shule za sekondari, hospitali, zahanati, vituo vya afya, pampu za maji na maeneo mengine muhimu ya huduma za kijamii.

Alisema awamu hiyo ya tatu, itaanza katika mwaka 2016/17 na kukamilika mwaka 2018/19.

Vijiji 8,000 vinatarajiwa kupatiwa umeme chini ya mradi wa REA Awamu ya Tatu. Wakati huo huo, Kamati hiyo ya Bunge kupitia kwa Mwenyekiti wake, Dotto Biteko imeipongeza Wizara ya Nishati na Madini kwa ukusanyaji wa maduhuli kwa kipindi cha nusu mwaka na kueleza kuwa mwelekeo wa ukusanyaji huo, unakwenda vizuri.

Awali, akiwasilisha taarifa ya wizara kuhusu upatikanaji wa fedha na utekelezaji wa majukumu kwa kipindi cha nusu mwaka kwa Kamati, Katibu Mkuu wa wizara, Profesa Justin Ntalikwa alieleza kuwa hadi kufikia Desemba 31 mwaka jana, wizara ilikuwa imekusanya jumla ya Sh bilioni 201.86 sawa na asilimia 54.46 ya lengo lililokusudiwa.

Sambaza Makala hii: Share on Facebook0Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn0Share on Google+0Email this to someone

You may also like

0 comments

By