Habarika | MAKONDA ATANGAZA NEEMA KWA WATUMISHI WA SERIKALI NA TAASISI ZA UMMA
layout-wrap boxed
Tuesday, May 22, 2018

MAKONDA ATANGAZA NEEMA KWA WATUMISHI WA SERIKALI NA TAASISI ZA UMMA

Wafanyakazi wa serikali na taasisi za umma mkoa wa Dar es Salaam wapo mbioni kupata mikopo nafuu ya ujenzi wa nyumba katika maeneo yao.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akihutubia maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ngazi ya Mkoa kwenye Uwanja wa Uhuru.

“Tunajua wengi wenu mna viwanja lakini kuingia katika ujenzi ni kazi ngumu sana, hivyo kama mkoa tumewatafuta watu ambao watatujengea nyumba hizo kwa gharama nafuu kabisa ndani ya miezi sita na kutukabidhi nyumba hizo,” alisema Makonda.

Makonda alisema nyumba hizo zitajengwa katika viwanja na maeneo ambayo wafanyakazi wenyewe wanamiliki viwanja hivyo na wanafanya hivyo ili kumsaidia mtumishi kuepukana na gharama kubwa za ujenzi pamoja na hali ya maisha iliyopo sasa.

Alisema pindi ujenzi utakapokamilika watumishi watalipia gharama kidogo kidogo hadi kumaliza mikopo yao hiyo ya ujenzi na patakuwa na ramani tofauti tofauti.

Aidha, aliwataka wafanyakazi kufanya kazi kwa bidii ili kuleta tija na hata watakapoomba nyongeza ya mishahara basi mwajiri aone ipo haja ya kufanya hivyo kulingana na kazi unayoifanya.

Mapema katika hotuba ya wafanyakazi mkoa wa Dar es Salaam iliyoandaliwa na Shirikisho la Wafanyakazi la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli (TRAWU) Mkoa, Elias Chizingwa alisema wafanyakazi hasa katika sekta ya elimu wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo mazingira ya kufanyia kazi.

Chizingwa alisema ipo haja kwa mkoa kufanya jitihada za makusudi na za haraka kuboresha mazingira ya kazi hasa kwa upande wa elimu kwa kuboresha mazingira ya kufundisha na kufundishia.

Aidha, alisema watumishi wa Reli kutoka Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) na Kampuni ya Reli (TRL) wanadai malimbikizo ya mishahara yao hivyo wanaomba aingilie kati na kufanikisha utatuzi wa kero hiyo.

Makonda aliahidi kuingilia kati matatizo hayo ya wafanyakazi na kuyatafutia utatuzi na amewaambia watumishi wa Jiji la Dar es Salaam juu ya kuanzisha dawati maalumu la kusikiliza kero zinazohusu wafanyakazi kila Alhamisi.

Aidha, kuhusu upande wa changamoto za elimu amesema mkoa upo mbioni kufanya harambee kwa ajili ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kununulia madawati na kufanikisha ujenzi wa madarasa na kuwaomba wadau mbalimbali kujitokeza ili kufanikisha adhma yake hiyo.

 -HabariLeo
Sambaza Makala hii: Share on Facebook1Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn0Share on Google+0Email this to someone

You may also like

0 comments

By