Habarika | Makala
layout-wrap boxed
Sunday, April 22, 2018

Makala

Kutokana na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia, kwa sasa maisha yamerahisishwa sana. Huna haja ya kutumia nguvu kubwa sana kutafuta bidhaa. Unaweza kukaa ndani tu na ukafanya manunuzi yako kwa kutumia simu yako ya mkononi tu na bidhaa ikakufikia popote ulipo bila hata ya kutoa jasho. Huo ndio urahisi ambao huduma ya M-PAPER inakuletea.

M-PAPER ni nini?

M-PAPER ni huduma ambayo inakufanya wewe mfuatiliaji wa habari kwa njia ya magazeti na majarida, kusoma magazeti na majarida uyapendayo kwa kutumia simu yako ya mkononi ambapo utaweza kusoma ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho kwa nusu bei ya gazeti halisi. Kwa mfano kama gazeti halisi unalonunua mtaani linauzwa Sh 1000/= basi ukilinunua na kulisoma kupitia M-PAPER litakuwa na gharama ya Sh 500/= tu.

Ni magazeti/majarida yapi yanapatikana kwenye huduma hii ya M-PAPER?

Kupitia App ya M-PAPER utaweza kusoma magazeti mbali mbali kama vile Tabibu, Uhuru, Rai, Tanzania Daima, HabariLeo, The Citizen, Majira, JamboLeo, Daily News, Mtanzania, Raia mwema, Mzalendo, Mwanahalisi na pia yakiwemo magazeti yako pendwa ya Michezo na Burudani kama vile Dimba, Bingwa, Mwana Soka na SpotiLeo.

Unawezaje kuipata huduma ya M-PAPER?

Huduma hii inapatikana kwa njia kuu MBILI ambazo ni mtandaoni kupitia link ya www.mpaper.co.tz au kwa kudownload App iitwayo M-PAPER inayopatikana Google Store kwa wale watumiaji wa simu za Android na App Store kwa wale watumiaji wa simu zinazotumia mfumo wa iOS.

Nawezaje kujiunga na huduma hii ya M-PAPER?

Zifuatazo ni hatua za kujiunga na huduma ya M-PAPER kupita ile njia ya ku-download app..Soma maelezo kisha husishanisha na picha inayoonekana chini kwa mifano zaidi. (Kwa simu za Android tu)

bakari1

 1. Ingia kwenye Google Play au App Store kwenye simu yako ya mkononi kisha andika M-PAPER kisha bonyeza INSTALL
 2. Baada ya ku-install app kwenye simu yako, Chagua Lugha kati ya KIINGEREZA au KISWAHILI
 3. Baada ya hapo ingiza naomba yako ya simu kwa wale watumiaji wa mtandao wa Vodacom
 4. Ukishaweka namba ya simu, utatumiwa namba ya uthibitisho kwa njia ya SMS kwenye namba yako ambapo utaweka namba hiyo uliyotumiwa kwenye sehemu unayotakiwa kujaza
 5. Baada ya hapo sasa utaweza kuyaona magazeti yote na majarida yanayopatikana.

 

Nawezaje kununua gazeti au jarida baada ya kujiunga?

Utaweza kununua gazeti kupitia M-PAPER baada ya kuongeza salio kwenye akaunti yako kwa kutumia akaunti yako ya M-Pesa, muda wa kawaida wa maongezi (Airtime) AU kupitia kadi zako za malipo za benki (Credit Cards) kama inavyoonekana kwenye picha namba moja hapo chini.

bakari2

Kuongeza salio kupitia kwenye akaunti yako ya M-Pesa fuata utaratibu kama inavyoonekana kwenye picha namba tatu hapo chini ambazo ni:

 1. Piga *150*00#
 2. Chagua 4 Lipa kwa M-Pesa
 3. Chagua 3 kwenye orodha
 4. Chagua 5 Vodacom
 5. Chagua 4 M-Paper
 6. Weka namba yako ya Kumbukumbu ambayo utaiona ukibonyeza akaunti yangu Mfano:( 117524)
 7. Weka kiwango
 8. Weka PIN Kulipa
 9. Utapokea ujumbe wa udhibitisho wa malipo.

Kuongeza salio kupitia Salio la kawaida kwenye simu yako, utatakiwa kubongeza kitufe cha Muda wa Maongezi kwenye picha namba moja hapo chini, kisha utaweka kiasi unachotaka kuongeza kama inavyooneka kwenye picha namba mbili, na vivyo hivyo kwa kutumia credit cards kama inavyoonekana kwenye picha namba nne hapo chini ambapo utachagua huduma unayotaka kutumia

Unaweza kusoma magazeti yote ya siku/wiki/mwezi husika bila kikomo kwa kununua vifurushi vya siku, wiki au mwezi kama inavyooneka kwenye picha namba tano hapo chini ambapo kifurushi cha wiki kitagharimu Sh 499/=, cha mwezi Sh 2,999/= na cha mwezi Sh 11,999/=

NB:

Mchakato wote huu wa kujiunga na M-PAPER ni kwa simu za Android tu, tutazungumzia mchakato kwa wale watumiaji wa iPhone siku nyingine.

Kama wewe sio mtumiaji wa mtandao wa Vodacom, unaweza kujiunga kupitia Facebook au Email na ukafanya malipo kupitia credit cards au ukatumiwa salio kutoka M-Pesa na rafiki yako mwenye namba ya Vodacom kuja kwenye namba yako.

Nyayo zilizoachwa na binadamu wa kale mamilioni ya miaka iliyopita zimegunduliwa nchini Tanzania karibu na pahala ambapo nyayo sawa na hizo ziligunduliwa miaka ya 1970.

Alama hizo za miguu ziliachwa na binadamu wa kale walipotembea kwenye matope na majivu ya volkano yaliyokuwa hayajakauka.

Wataalamu wanakadiria kwamba viumbe ambao hujulikana kama Australopithecus afarensis, ndio walioacha nyayo hizo, na walikuwa na kimo na unene uliotofautiana ambapo wanasayansi hao wanasema nyayo hizo zinaashiria jinsi binadamu wa kale walivyoishi.

Australopithecus afarensis ni miongoni mwa aina ya binadamu wa kale wanaofahamika zaidi na ambao waliishi kipindi kirefu.

Visukuku vya “Lucy”, mwanamke kijana aliyeishi Ethiopia zaidi ya miaka 3.2 milioni, ndiye maarufu zaidi kutoka kwa kundi hilo la binadamu.

Nyayo hizo zilizogunduliwa huenda ziliachwa na mwanamume aliyekuwa labda anatembea na wenzake wa kike wadogo kwa kimo.

“Ushahidi huu mpya, ukiuzingatia pamoja na ushahidi wa awali, unaashiria kwamba binadamu wa kale walikuwa wanatembea kama kundi kwenye mandhari ambapo kulikuwa na matope, majivu na mawe ya volkano baada ya kulipuka kwa volkano na mvua kunyesha. Lakini kuna zaidi,” amesema mtafiti mkuu Prof Giorgio Manzi, mkurugenzi wa mradi huo wa akiolojia nchini Tanzania.

“Nyayo za mmoja wa binadamu kati ya zile tulizogundua ni kubwa kuliko za wengine katika kundi hilo, jambo linaloashiria kwamba huenda alikuwa mwanamume.

“Kusema kweli, kimo cha 165cm ambacho kinadokezwa na nyayo hizo kinamfanya kuwa moja wa binadamu wa Australopithecus warefu zaidi kugunduliwa hadi wa leo.”

Maisha kama ya sokwe

Mwaka 1976, nyayo zilizohifadhiwa ambazo zinaaminika kuachwa na Australopithecus ziligunduliwa karibu na Laetoli, kaskazini mwa Tanzania, takriban kilomita 40 kutoka Olduvai Gorge.

NyayoNyayo hizo ziliachwa kwenye majivu ya volkano

Nyayo hizo ambazo zinakadiriwa kuachwa miaka 3.66 milioni iliyopita, ni miongoni mwa nyayo za kale zaidi kugunduliwa duniani.

Sasa, ugunduzi wa kundi la sasa la nyayo umefichuliwa kwenye jarida la eLife.

Nyayo hizo ziligunduliwa wakati wa ufukuzi kwa ajili ya kujengwa kwa makumbusho eneo lililo mita 150 kusini mwa eneo ambalo ugunduzi wa kwanza ulifanywa.

Watafiti walioongoza uchunguzi huo, ambao wanatoka Italia na Tanzania, wanafikiri huenda nyayo hizo zina uhusiano, na zinaashiria mtindo wa maisha wa Australopithecus.

“Nadharia ambayo ni ya kuaminika ni kwamba kundi hilo labda lilikuwa na mwanamume mmoja, mwanamke mmoja au wawili au watoto, jambo ambalo linatufanya tuamini kwamba mwanamume huyo – alikuwa (alijamiiana) na wanawake zaidi ya mmoja,” anasema Dkt Marco Cherin, mkurugenzi wa kitivo cha utaalamu wa mifupa ya kale katika Chuo Kikuu cha Perugia, Italia.

Ugunduzi huu unadokeza kwamba huenda mtindo wao wa kuishi ulikuwa “unakaribiana zaidi na wa sokwe kuliko sokwe-mtu au binadamu wa sasa,” wanasema.

Nyayo hizo zinafanana na za mwanadamu

Miongoni mwa sokwe, sokwe dume na sokwe jike kadha huunda kundi la kujamiiana na kulea watoto.

Utafiti huo umeibua maswali kuhusu ni vipi na ni lini binadamu walipoanza kutembea wanavyotembea sasa.

Kutembea wima kwa miguu miwili

Australopithecus waliweza kutembea wakiwa wamesimama wima kwa miguu yao miwili, lakini hatujui walifanana kwa kiasi gani na binadamu wa sasa kwa jinsi walivyotembea.

Prof Robin Crompton wa Chuo Kikuu cha Liverpool, ambaye hakuhusika katika utafiti huo, anasema nyayo hizo zilizogunduliwa majuzi zitatoa maelezo zaidi, utathmini wa takwimu utakapofanyika.

“Baadhi ya watu wanasema walikuwa na mwendo tofauti kiasi, lakini sifikiri kwamba kuna ushahidi mzuri kuhusu hilo,” ameambia BBC.

“Iwapo wanadamu wamekuwa wakitembea kwa mwendo sawa na wa sasa kwa zaidi au chini ya miaka 3.65 milioni, na mababu wa binadamu – katika kundi jingine la viumbe – Australopithecus – basi hilo linashangaza sana”

Biashara ya Bodaboda imeshamiri katika Jiji la Dar es Salaam lenye wakazi zaidi ya milioni nne. Hata hivyo, licha ya ukweli kwamba helmeti kupunguza kwa asilimia 69 hatari ya mwendesha pikipiki kuumia kichwa pale apatapo ajali, na kapunguza kifo kwa asilimia 42, uvaaji wa helmeti kwa madereva na abiria wao bado ni kitendawili.

Kamanda wa Usalama Barabarani Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Awadhi Haji anasema wameshatoa elimu ya kutosha kwa waendesha pikipiki ili wahakikishe wanavaa kofia ngumu pamoja na abiria wao wakati wanapopanda pikipiki.

“Watakaokaidi agizo tutawakamata madereva na abiria wao na kuwafikisha mahakamani. Huko wanaweza kutozwa faini inayoanzia Sh 300,000 au kufungwa jela kati ya miezi sita au mwaka mmoja kutokana na sheria ya Sumatra,” anasema kamanda Haji.

Polisi wameamua kufanya hivyo kutokana na faini ya Sh 30,000 chini ya sheria ya usalama barabarani kutowaogopesha madereva wengi wa pikipiki. Ndiyo maana sasa uamuzi ni kuwapeleka mahakamani.

“Huko tunawashitaki chini ya sheria ya Sumatra na operesheni hii tunaifanya kwa kushirikiana na Sumatra wenyewe,” anasema ACP Haji.

Gasper Athony wa Chuo cha Future World kinachotoa mafunzo kwa madereva wa pikipiki kwa kushirikiana na Chuo cha Mafunzo Stadi (Veta), anasema zimethibitisha kwamba wapanda pikipiki wasiovaa helmeti wanapoanguka wanaumia zaidi kuliko wale waliovaa helmeti.

“Idadi ya waliojeruhiwa kichwani wakati wamevaa helmeti ni ndogo ukilinganisha na idadi ya watu waliojeruhiwa kichwani wakiwa hawakuvaa helmeti. Kofia hizi ni muhimu kwa dereva na abiria wa Bodaboda,” anasema Antony.

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2015 inaielezea Tanzania kwamba usimamizi wa vihatarishi vya uvaaji wa helmeti hapa nchini unatekelezwa alama 4 kati ya alama 10.

Hii maana yake ni kwamba Mamlaka zinazosimamia usafiri hapa nchini hususan Jeshi la Polisi na Sumatra zinatekeleza kwa kiwango cha chini katika kuhakikisha sheria zinafuatwa na waendesha Bodaboda linapokuja suala la uvaaji wa helmeti.

Kwa mujibu wa Antony, ambaye ni mkufunzi wa madereva wa Bodaboda, uvaaji wa helmeti unapunguza kujeruhiwa kichwani mara tatu.

“Sehemu ngumu ya nje inazuia kupenya kwa kitu chochote na sehemu ya ndani ya kofia hiyo inasaidia kupunguza mgandamizo. Hali kadhalika, helmeti nyingi zina sehemu ya kukinga macho dhidi ya vumbi, upepo na kuzuia wadudu wanaoruka, hivyo dereva kuendesha pikipiki bila kuvaa helmeti anaweka maisha yake na ya abiria katika hatari kubwa,” anasisitiza Antony.

Kuna aina nne za helmeti na ya kwanza ni Full Face ambayo inafunika uso wote, pili ni aina ya Motor Cross ambayo nayo inafunika kichwa chote pamoja kidevu.

Aina ya tatu ni Modula ambayo inafunika kichwa; lakini inakuwa na kioo cha kufunua na ya mwisho ni Open Face ambayo inafunika kichwa lakini haina kioo mbele.

Robert Mnyambe, mmoja wa madereva wa bodaboda mjini Morogoro, anakiri kwamba madereva wengi wa pikipiki hawapendi kuvaa helmeti kwa madai kwamba uvaaji wa kofia hiyo ngumu unapunguza uwezo wa kuona na kusikia vizuri hivyo kusababisha ajali nyingi.

Kwa upande wa abiria, Mnyambe anasema wengi wa abiria; hasa wanawake hawataki kuvaa helmeti kwa sababu mbalimbali.

Kuna madai ya kuogopa kuchangiana jasho kwa vile zinavaliwa na abiria wengi. Kubwa zaidi ya madai ya abiria wanawake ni eti kwamba helmeti zinavuruga nywele zao ambazo wanatumia gharama kubwa kuzitengeneza.

Mfano mzuri ni Neema Wema mkazi wa Dar es Salaam, yeye hukataa kuvaa helmeti eti kwa kuwa anahofia kuambukizwa magonjwa ya ngozi kutokana na kofia hizo kutumiwa na abiria walio wengi.

“Kofia za hawa bodaboda hawazifanyii usafi. Zinanuka. Ndio maana sivai,” anasema Neema na kuongeza, “Dar es Salaam ni joto kali, ukiivaa kofia hii lazima tu utaivua maana inaleta joto na hiyo kuwa na harufu kali.”

Dereva mwingine wa bodaboda, James Kemege, na ambaye anafanya biashara hiyo kwa mwaka wa tatu sasa anasema: “Mimi nina helmeti mbili ya kwangu na abiria. Lakini abiria wengi hawataki kuvaa helmeti hasa wanawake kwa madai kuwa nywele zao zinaharibika pia wanadai zina uchafu.”

Kemege anasema abiria wake wanadai helmeti zinaambukiza ugonjwa wa ngozi, mba. Anaasema wanadai wanaogopa kuambukizwa magonjwa ya ngozi kutokana na kofia hiyo kuvaliwa na watu wengi. Kwa mawazo yake Kemege, serikali iwachukulie hatua abiria wanaokataa kuvaa helmeti ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani.

“Sisi madereva tukikosea tunapelekwa mahakamani. Iwe vivyo hivyo pia kwa abiria. Na watozwe Sh 50,000 wanapokutwa na hatia sawa na dereva.”

Lakini, Anneth Mwakajumba anasema abiria wengi hawavai kofia ngumu kwa sababu hakuna ufuatiliaji kutoka kwa polisi jambo ambalo abiria wanaona sio jambo la lazima kuvaa hiyo kofia.

“Sijawahi kuona polisi inamkamata mwendesha bodaboda ambaye hajavaa helmeti au abiria aliyekamatwa kwa kupanda bodaboda bila kuvaa helmeti. Kwa kuwa hakuna ufuatiliaji ndio maana watu wengi wanapuuzia kuzivaa, lakini polisi wakikomaa abiria tutavaa tu kwa lazima maana ni kwa manufaa ya maisha yetu,” anasema Anneth.

Dk Mariam Kalomo, wa Kitengo cha Tiba, Wizara ya Afya, anaeleza kofia ngumu zinapovaliwa na abiria mbalimbali zinaweza kuambukiza magonjwa ya ngozi kama malengelenge, fungasi na seabies.

“Sisi madaktari tunawashauri wateja wa bodaboda wawe na tabia ya kununua kofia zao kama hawataki kuambukizwa hayo magonjwa. Lakini pia ni afadhali maambukizi kwa kuwa yanatibika kuliko upate ajali ambayo inapelekea kifo,” anasema Dk Kalomo.

Hata hivyo, hakuna takwimu za watu waliougua magonjwa ya ngozi kwa kuvaa helmeti. Mkurugenzi wa Global Helmet Vaccine Initiative (GHVI), Alpherio Nchimbi, anasema utafiti uliofanywa na na taasisi yake katika mikoa ya Tanga, Morogoro na Dar es Salaam unaonesha kuwa wanaume wengi wanavaa helmeti kuliko wanawake.

“Wanaume wanaovaa helmeti ni zaidi ya mara nne ya wanawake, hii inadhihirisha kwamba wanawake hawapendi kuvaa kofia ngumu na hata akipewa na dereva yuko radhi kuishikilia mkononi,” anabainisha Nchimbi. Anashauri kwamba wateja wa bodaboda wapewe elimu ili kila mtu anunue kofia ngumu na kukaa nayo ndani.

“Kila nyumba ina mwavuli licha ya kuwa sio wakati wote mvua zinanyesha. Ifikie wakati kila nyumba iwe na kofia ngumu ili siku itakapolazimu kupanda pikipiki atumie ya kwake.”

Wazo hili linaungwa mkono na abiria Flora Kamage, kwamba abiria wanaoutumia zaidi usafiri wa pikipiki waone umuhimu wa kununua kofia zao. Hii ni itasaidia kujikinga na uchafu na magonjwa ya ngozi kwa kutumia kofia inayotumiwa na watu wengi.

Ofisa Mfawidhi wa Sumatra mkoani Iringa, Patel Ngereza, anasema dereva wa bodaboda atatakiwa kuvaa kofia kwa ajili ya usalama wake na abiria. Kwa maelezo ya Ngereza, sheria ya ulipaji wa leseni ya bodaboda iliyopitishwa na Bunge mwaka 2011, inapaswa kutumika ipasavyo, ili kuzuia ajali zinazosababishwa uzembe wa madereva.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoani Iringa, Leopold Fungu , anasema polisi wa kikosi hicho wamekuwa wakiwakamata na wataendelea kuwakamata madereva wa Bodaboda na wengine ambao hawazingatii sheria za usalama barabarani na sheria nyingine za nchi.

Fungu anasema madereva wengi wa bodaboda wamekuwa wakikamatwa kwa makosa makubwa saba ambayo ni pamoja na kuendesha chombo hicho bila kuwa na leseni, wakiwa wamelewa, hawajavaa helmeti, wamevaa viatu vya wazi, mwendo kasi na kubeba abiria zaidi ya mmoja na baadhi kubeba watoto wakati sheria hairuhusu.

Sheria ya usafirishaji wa Pikipikiya Sumatra hairuhusu mtoto wa chini ya miaka 8 haruhusiwi kupakiwa kwenye pikipiki bila msaada wa mtu mwingine.

Licha ya kampuni za kutengeneza helmeti kutengeneza kofia ngumu kwa watoto, lakini hapa nchini sheria imenyamaza kuhusu kofia ya mtoto aliyepanda na kusaidiwa na mzazi. Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani mkoani Morogoro, Boniface Mbao, anakiri kuwa kutovaa helmeti ni tatizo kubwa mkoani kwake.

Wanachofanya ni kuendelea kuwakamata madereva wakaidi lakini pia wanatoa elimu.

“Uelewa wa helmeti bado ni mdogo ndio maana tumekuwa tunafanya operesheni kubwa na tunapowakamata mbali l ya kuwalipisha faini, tunawaelimisha umuhimu wa kuvaa helmeti na faida zake,” anasema Kamanda Mbao.

Chanzo: Habari Leo

Utafiti uliofanywa na wanasayansi wa Japan umethibitisha kwamba kukaa kwa mda mrefu na kutazama vipindi vya televisheni kwa masaa mengi kunahatarisha afya kwani huhusishwa na maradhi yanasababisha mzunguko wa damu mwilini kutokuwa sawa.

Watafiti hao wanasema, hali hiyo pia huenda ikasababisha damu kuganda na kutengeneza vidonge katika sehemu kama vile miguu, na iwapo mgando huo utasukumwa na nguvu za mzunguko wa damu na kuingia sehemu kama vile mapafu, husababisha vifo.

Utafiti huo ulihusiha watu zaidi ya 86,000 ambao hupendelea kutazama televisheni katika mida mbalimbali kwa siku kisha afya zao zilifuatiliwa kwa zaidi ya miaka 19 tangu mwaka 1988

Matokeo yalikuwa kila muda wa masaa mawili yalipopita mtu akikaa kutazama televisheni, nayo hatari ya kupata ugonjwa huo wa mapafu uitwao ‘Fatal pulmonary embolism’ ulioongezeka kwa asilimia 40%.

Iligundulika pia kuwa waliotazama vipindi vya televisheni kwa zaidi ya saa 5 walikuwa katika hatari zaidi kuliko waliotazama televisheni kwa mda wa chini ya saa 3.

Zaidi ya hayo watu huambatanisha kitendo cha kukaa na kutazama televisheni huku wakila vitafunio kama vile Popcorns na Crisps ambavyo pia huwasababishia si tu mwili kukosa mazoezi bali pia kuongezeka kwa uzito unaohatarisha afya.

Chanzo: BBC Swahili

Ripoti mpya inasema watoto wanaonyonya vidole au kung’ata kucha zao kwa meno huenda wasipate matatizo ya kuathirika kutokana na mazingira hewa au kula vyakula fulani.

Kwa mujibu wa waandishi katika jarida la Pediatrics, huo ni usafi dhanio ambao huimarisha mfumo wa kinga ya mwili.

Unyonyaji wa kidole gumba na ung’ataji wa kucha umeonekana kuzuia baadhi ya alergy.

Kati ya watu elfu moja wenye umri wa kati ya miaka mitano hadi thelathini na mbili,walifanyiwa uchunguzi kwa muda nchini New Zealand.

Lakini tabia hii ya unyonyaji vidole na ung’ataji kucha haisaidii watu wenye pumu au mtu anapopata homa kali.

Uchunguzi uliofanywa na kurekodiwa kwa watoto wenye umri wa kati ya miaka mitano na kumi na moja na wengine waliofanyiwa vipimo ni wenye umri kati ya miaka kumi na tatu na thelathini na miwili huku theluthi moja ya watoto hao ni wanyonyaji wa vidole mara kwa mara au hung’ata kucha zao na katika vipimo walivyofanyiwa watoto hao wameonekana kuwa wana kiwango kidogo cha kuathirika kutokana na mazingira hewa au kula vyakula fulani.

Watoto wanaoweza kupata matatizo ya kuathirika kutokana na mazingira hewa au kula vyakula fulani (alergy) hutokana na vitu kama vumbi kutoka majumbani,manyoya ya paka au mbwa, lakini watoto wenye kunyonya vidole gumba na kung’ata kucha walikuwa ni chini ya theluthi moja kuliko watoto wasio na  tabia hii ya unyonywaji vidole.

Na tabia hii ya unyonyaji vidole au ung’ataji kucha inaonekana kuwa kinga mpaka wanapofikia umri wa utu uzima.

” kuwa na paka au mbwa majumbani, ndugu au jamaa wanaofanya kazi mashambani pia imeonekana kuwa ni sababu kubwa inayosababisha mazingira ya ukuaji wa magonjwa yanayosababishwa na kuathirika kutokana na mazingira hewa au kula vyakula fulani.

-BBC SWAHILI

Tumesikia kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda lakini pia Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa wamepiga maarufuku biashara ya shisha jijini Dar es Salaam kwa maelezo kuwa ina madhara makubwa sana ikiwa ni pamoja na kupoteza nguvu kazi ya taifa.

Haya bi baadhi ya madhara yatokanayo na uvutaji wa shisha.

1.Shisha husababisha Saratani (Cancer). Kutokana na moshi mwingi ambao mvutaji huvuta kwa muda wote anapokuwa anavuta shisha, unamuweka kwenye hatari ya kupata saratani.  Hata baada ya kupita kwenye maji ambayo hudai kuwa huondoa sumu, moshi ule bado una kemikali nyingi kama Carbon Monoxide ambazo ni hatari.

Mtumiaji anaweza kupata saratani ya Koo, Kibofu au Mapafu, Mtu kivuta shisha kwa saa moja, moshi anaokuwa amemeza ni sawa na aliyevuta sigara katika ya 100-200.

2. Shisha husababisha matatizo ya moyo. Tumbaku na moshi unaokuwepo pindi mtu anapovuta shisha, unaelezwa kuwa husababisha matatizo katika mishipa ya damu iliyopo kwenye moyo.

3. Uvutaji wa shisha husababisha matatizo ya meno (Periodontal disease)- Uvutaji wa shisha huathiri periodontal tissue ambapo pindi zinapoathiriwa husababisha matatizo ya meno na wakati mwingine hata mpangilio wa meno mdomoni huvurugika.

4. Kutokana na mabomba yanayotumika kuvutia kwenye baa na migahawa kutosafishwa vizuri, wakati mwingine shisha huweza kusababisha maambukizi ya magonjwa kama vile Kifua Kikuu (TB) unezaji wa fungus zinazoathiri mapafu, na vijidudu vinavyosababisha vidonda vya tumbo.Wakati mwingine wavutaji hutumia bomba moja bila hata kulisafisha kabisa, hii ni hatari kwa afya ya wavutaji hao.

5. Hupekelea mama mjamzito kujifungua mtoto mwenye upungufu wa uzito kama atakuwa anavuta shisha akiwa majamzito. Mbali na hili uvutaji shisha huathiri mfumo wa upumuaji wa mtoto atakayezaliwa.

6. Mathara ya shisha hayapo tu kwa yule anayevuta, ila hata yule aliyepokaribu na anayevuta huathrika sana kama, wataalamu wameeleza kuwa mtu wa pembeni wakati mwingine huathirika kuliko hata ambaye huvuta sigara.

7. Shisha pia husababisha mtu kuwa na ngozi iliyokunjamana (yenye makunyanzi). Kijana wa miaka 20 akiianza kutumia shisha, baada ya muda ngozi yake itakuwa iliyokunjama kama ya mzee.

8. Shisha husababisha upungufu wa nguvu za kiume ambapo wanaume wengi hushindwa kufanya tendo la ndoa kwa muda mrefu. Hii wakati mwingine husababisha mwanamke kutoka nje ya ndoa au hata ndoa kuvunjika.

-SwahiliTimes

Watoto milioni 69 walio na umri wa chini ya miaka mitano duniani watapoteza maisha kwa magonjwa yanayoweza kuzuilika, watoto milioni 167 wataishi kwenye dimbwi la umasikini huku watoto wengine milioni 750 wako hatarini kuolewa wakiwa na umri wa utoto ifikapo mwaka 2030, imeelezwa.

Ripoti ya mwaka ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) imeeleza hatari hiyo kwa watoto inatokana na serikali za nchi zao, nchi wahisani na jumuiya za kimataifa kutokuweka juhudi na mipango yoyote ya kushughulikia tatizo hilo.

“Kushindwa kuwajali mamilioni ya watoto hawa ili waweze kuwa na maisha mazuri sio athari kwa watoto hao peke yake, bali ni hasara ambayo jamii yote itaishuhudia kwa siku za mbele,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Unicef, Anthony Lake na kuongeza; “Tuna uchaguzi wa kufanya, kuwekeza kwa watoto hao sasa au turuhusu dunia inayokuja iwe na matabaka ya kijamii pasipo usawa.”

Ripoti hiyo iliyotolewa jana New York, Marekani imesema kuna haja ya kuweka mikakati itakayosaidia watoto waende shule pamoja na kuwainua ili waondoke kwenye dimbwi la umasikini.

Alisema takwimu za dunia zinaonesha kuwa vifo vya watoto wa chini ya miaka mitano vinaongezeka kuliko ilivyokuwa miaka ya 1990, wavulana na wasichana wanakwenda shule kwa usawa katika nchi 129, lakini watu katika nchi hizo wanaishi katika umasikini wa hali ya juu, idadi inayokadiriwa kuwa nusu ya ile ya miaka ya 1990.

Ripoti hiyo imeeleza watoto ambao ni masikini zaidi idadi yao imeongezeka mara mbili zaidi na wako hatarini kupoteza maisha kabla ya kufikisha miaka mitano.

Maeneo ya kusini mwa Bara la Asia na Kusini mwa Jangwa la Sahara, idadi ya watoto wanaozaliwa na mama zao ambao hawana elimu idadi imeongezeka mara tatu na wako hatarini pia kupoteza maisha wakiwa chini ya umri wa miaka mitano kuliko wale ambao wanazaliwa na mama ambao wana elimu walau ya sekondari.

Wasichana ambao wanatoka kwenye kaya masikini zaidi nao wameongezeka mara mbili kuliko idadi ya wasichana ambao wanazaliwa kwenye familia zenye kipato cha kati.

Hali ni mbaya zaidi katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambako ripoti hiyo imefafanua kuwa walau watoto milioni 247 wanaishi kwenye umasikini mkubwa. Inaelezwa kuwa asilimia 60 ya watu wenye umri kati ya miaka 20 na 24 kutoka kaya masikini wamepata elimu ya msingi chini ya miaka minne.

Utafiti mpya unaonyesha matukio yanayoongezeka ya watu kunenepa kupitia kiasi huchangia kukua kwa tatizo la utapia mlo.

Kawaida utapia mlo umehusishwa na upungufu mkubwa wa chakula lakini utafiti huu umedhihirisha kuwa ulaji wa vyakula visivyo bora kwa afya, husababisha ulimbikizaji wa sukari, chumvi na mafuta ya cholesterol huku mwili ukipungukiwa na madini muhimu yanayohitajika ili kujenga siha na afya njema.

Ripoti hiyo inaonya kuwa iwapo hatua mwafaka hazitachukuliwa kukabiliana na tatizo la uzito kupindukia litapelekea kudorora kwa viwango vya hali ya afya duniani.

Utapia mlo umekuwa ukihusishwa na watoto ambao hawana chakula hawakui na kwamba wanakabiliwa na maambukizi.

Haya bado ni maswala makuu, lakini kuna maendeleo yalioafikiwa katika sekta hiyo. Ripoti hiyo inatoa changamoto zinazosababishwa na kunenepa kupitia kiasi.

Ongezeko la watu wanene kupitia kiasi limeanza kuonekana katika kila nchi ulimwenguni

Mamia ya mamilioni ya watu huugua utapia mlo kwa sababu ya kuwa na sukari nyingi,chumvi na mafuta katika miili yao,ripoti hiyo imesema.

-BBC

Shirika moja la kimataifa limesema ushindi wa Donald Trump unachukuliwa kuwa miongoni mwa hatari 10 kuu zaidi zinazokabili dunia.

Shirika hilo la Economist Intelligence Unit linaonya kuwa iwapo Bw Trump atashinda urais Marekani, hilo huenda likavuruga uchumi wa dunia na kuongeza hatari za kisiasa na kiusalama dhidi ya Marekani.

Hata hivyo, shirika hilo halimtarajii Bw Trump, anayeongoza kwenye kinyang’anyiro cha kumchagua atakayepeperusha bendera ya chama cha Republican, kumshinda Bi Hillary Clinton ambaye shirika hilo linasema “ana uwezekano mkubwa sana kuwa mgombea wa chama cha Democratic”.

Ushindi wa Trump unaorodheshwa kuwa hatari zaidi kwa dunia kushinda hata Uingereza kuondoka kutoka kwa Umoja wa Ulaya au hata makabiliano ya kivita katika bahari ya South China Sea.

Kuyumba kwa uchumi wa Uchina au Urusi, kuingilia kivita Ukraine na Syria na kusababisha “vita baridi” vipya ni miongoni mwa mambo ambayo yanachukuliwa kuwa hatari zaidi ya ushindi wa Bw Trump.

“Kufikia sasa, Bw Trump ametoa maelezo machache sana kuhusu sera zake, na huwa anabadilisha sana msimamo wake,” EIU wanasema kwenye ripoti yao ya tathmini ya hatari zinazoikabili dunia ambapo tathmini hizo pia huangazia athari za jambo fulani na uwezekano wa jambo hilo kutokea

EIU hutumia kipimo cha moja hadi 25, na Bw Trump ana alama 12, sawa na hatari ya “kuongezeka kwa ugaidi wa kijihadi kuathiri uchumi wa dunia”.

“Amekuwa na msimamo mkali sana dhidi ya biashara huria, pamoja na Nafta, na ameituhumu Uchina mara nyingi kuwa taifa linalofanyia mchezo sarafu,” EIU inasema.

Shirika hilo limeonya kuwa matamshi yake makali dhidi ya Mexico na Uchina hasa yanaweza kusababisha vita vya kibiashara.

Bw Trump amependekeza ukuta ujengwe kati ya Marekani na Mexico kuzuia wahamiaji na pia ametetea kuuawa kwa jamaa za magaidi. Aidha, amependekeza kuvamiwa kwa Syria ili kuangamiza kundi la Islamic State.

EIU wanasema msimamo wake kuhusu mzozo Mashariki ya Kati pamoja na pendekezo kwamba Waislamu wazuiwe kuingia Marekani vinaweza kutumiwa na makundi ya itikadi kali za Kiislamu kuwatafuta wafuasi zaidi.

-BBC SWAHILI

Na Deusdedith Manugulilo,

Kwa mujibu wa ripoti ya kiuchumi Duniani iliyotolewa na benki kuu ya Dunia mwaka 2014 ilionesha Tanzania kuwa nchi ya 86 duniani katika ukuzaji wa pato lake la taifa.

Tanzania inajinasibu kukuza pato la taifa kwa takribani asilimia saba kwa miaka mitano iliyopita huku katika tafiti za kimataifa ikiendelea kuning’inia chini ya nchi nyingi zikiwemo zile ambazo zilikuwa na uchumi sawa miaka kadhaa nyuma.

Kwa mujibu wa ripoti ile ile ya benki kuu ya Dunia nchi ya Thailand inakamata nafasi ya 32 duniani ikiwa nafasi 54 mbele zaidi ya Tanzania katika ukuzaji wa pato lake la ndani la taifa.

Kabla ya hapo, mnamo mwaka 2011 benki ya Dunia iliitaja na kuitambua Thailand kama nchi yenye uchumi wa kati sawa sawa na nchi kama Brazil na Afrika Kusini.

Mnamo miaka ya 1970/80 Thailand ilikuwa na zaidi ya asilimia 70% ya wananchi wanaotegemea kilimo kama ajira na shughuli kuu ya kiuchumi nchini humo sawa sawa na Tanzania. Hii ndio ilikuwa shughuli kubwa ya ukuzaji wa pato la taifa katika nchi hizi.

Miaka kadhaa hali ilibadilika na hii ni mara baada ya wananchi wengi kutimkia mijini. Hivyo iliibidi nchi ya Thailand kufanya mapinduzi katika sekta nyingine ili kwenda sawa na mabadiliko hayo.

Kwanza Mapinnduzi makubwa yalihamia kwenye sekta kama Viwanda (migodi, umeme, ujenzi, maji na gesi). Sekta hizi pekee zilichangia asilimia 40 ya pato la taifa na kuweza kutengeneza takribani asilimia 17 ya ajira nchini Thailand.

thailand2

Kuonesha walidhamiria mabadiliko, vilianzishwa viwanda vya mazao ya chakula, vifaa vya umeme, kutengeneza magari na vipuli vyake, viwanda vya chuma na shaba. Pia mapinduzi mengine yalifanyika katika sekta kama biashara (kubwa na ndogondogo), utalii na usafirishaji ambazo kwa ujumla wake zimetoa ajira asilimia 51 na kuchangia pato la taifa kwa zaidi a asilimia 45.

Baadae kilimo nacho kilifanyiwa mapinduzi kuwa cha kisasa chenye kumthamini mkulima.na kilichangia asilimia 12 ya pato la taifa. Mazao makuu yakiwa kama mchele, nanasi, mihogo, mahindi, miwa na mazao ya uvuvi. Tanzania yanapatikana licha ya uzalishaji hafifu usio wa tija kwa mkulima na taifa kwa ujumla.

Kwa ujumla Thailand imehakikisha inafanya uzalishaji wa malighafi, mazao ya chakula na bidhaa kamili nyingi kama vifaa vya umeme na mashine zenye uwezo wa kushindana katika soko la dunia. Hii imetoa fursa ya ushindani ndani ya soko huria.

Je, Tanzania tunamhitaji kiongozi mwenye hekima kama za mfalme sulemani kutuvusha hapa tulipo? Au ndo kusema aliyelala zake ndoto tu??

 

MTAZAMO WANGU

Elimu lazima ipewe thamani ili iwe na uwezo wa kutoa wataalamu toshelezi kuendesha sekta tulizonazo. Uboreshwaji wa huduma ya elimu kwa jamii ikihusisha miundombinu na mitaala ya kufundishia ni muhimu hasa wakati huu elimu yetu inapotoa wahitimu badala ya wataalamu.

Ili ajira zipatikane na kupunguza wimbi la vijana wasio na ajira sekta kama viwanda, madini, mafuta na gesi ni lazima viboreshwe kwa kiwango toshelezi cha kutoa ajira kwa wingi. Pia kuweza kuzalisha malighafi na bidhaa zenye uwezo wa kushindana kwenye soko la dunia ili kumudu uchumi wa soko huria.

Kutoa fursa za kukuza mitaji ya wafanyabiashara wadogo wadogo na wakubwa lakini pia kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji kwenye sekta kama utalii na usafirishaji ziweze kutoa mchango chanya kwa wananchi na kukuza pato la taifa kama ilivyowezekana nchini Thailand kwa muda mfupi tu.

thailand3

Kuna sekta ambazo zinakua kwa kasi nchini Tanzania hivi sasa ambazo kwa Thailand hazijaoneshwa. Sekta hizo ni kama mawasiliano (vyombo vya habari na mitandao ya simu) na uchukuzi (Bandari, reli na mizani). Sekta hizi kwa nchini Tanzania zimetoa ajira kwa kiwango kikubwa na licha ya ufinyu wa usimamizi bado zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza pato la taifa na uchumi kwa ujumla.

Wahenga walinena “Asiyejua maana haambiwi maana” na “Kichwa cha kuku hakivikwi kilemba”.

NI HAYO TU.
Deusdedith Manugulilo
manugulilo@yahoo.com