Habarika | Kitaifa
layout-wrap boxed
Tuesday, May 22, 2018

Kitaifa

Waziri wa Fedha, Dr. Philiph Mpango amewaeleza Watanzania kila kilichosemwa kwenye mazungumzo IKULU na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia ambaye ameitembelea Tanzania ambapo moja ya vilivyojadiliwa ni Fly Over ya Ubungo ambayo itasaidia sana kuondoa foleni sugu.

Kulikuwa na mazungumzo rasmi yaliyofanyika IKULU na kubwa la kwanza ilikua ni kuihakikishia benki ya Dunia kwamba kwa kweli ni wabia wetu wazuri wa maendeleo na Rais amesisitiza kwa upande wa serikali tutaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na benki ya dunia.

Eneo moja ambalo Rais ameiomba Benki ya dunia itusaidie kuharakisha kuanza utekelezaji ni pale Ubungo kwenye makutano ya zile barabara.

Huu mradi wa Mabasi yaendayo kazi hautakuwa na ufanisi kama bado pale Ubungo utategemea Askari wa barabarani kuongoza magari kwahiyo Rais Magufuli amesisitiza zaidi.

Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia amekubali kwamba wataharakisha ule mchakato ili ujenzi wa barabara za juu kwenye makutano ya barabara Ubungo uanze.

Kuhusu gharama za ujenzi wa Fly Over Ubungo hatuna namba kamili kwa sasa kwasababu bado tunakamilisha majadiliano lakini kwa takwimu za awali haitapungua Dola za Kimarekani MILIONI 60.

 

Warusha matangazo ya televisheni na wenye vituo vya utangazaji wamependekeza matangazo ya bure yaondolewe na badala yake wananchi walipie.

Mapendekezo hayo yametolewa kwenye mkutano wa kukusanya maoni ulioandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa lengo la kuja na marekebisho ya gharama za kurusha matangazo ya televisheni ambayo huumiza pande zote.

Akichangia, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Agape Associates Limited wenye king’amuzi cha TING, Andy Fernandes alipendekeza vituo vya utangazaji viwalipe warusha matangazo (wenye ving’amuzi) dola za Marekani 2,500 (zaidi ya Sh milioni tano) kwa mwezi huku akisisitiza pia mlaji wa mwisho (mwananchi) alipie kiasi matangazo hayo.

“Wakati umefika sasa kwa mlaji wa mwisho (mwananchi) kulipa gharama za kuangalia matangazo ambazo zitamsaidia kumpunguzia makali mwenye kituo cha utangazaji, hata hospitali watu wanachangia,” alisema kauli iliyoungwa mkono na Kampuni za Star Media (T) Limited na Basic Transmission Limited ambao walipendekeza mwananchi alipie Sh 6,000 kwa mwezi.

Kwa upande wa vituo vya utangazaji, wao wamependekeza kuwepo na nafasi ya kufanya biashara kati yao na warusha matangazo, wapate fursa ya kuuza vipindi.

Edward Komba wa Abood Media alisema: “Vituo vilivyo mikoani vimekuwa na gharama kubwa ya kuandaa vipindi huku kukiwa na ugumu wa upatikanaji wa matangazo na kupendekeza vituo vilipe shilingi laki sita kwa warusha matangazo kwa mwezi.”

Sylvia Mushi wa Capital Television alipendekeza warusha matangazo wanunue vipindi kutoka kwenye vituo vya utangazaji na wao kupata fedha za kujiendesha kwa kumtoza mwananchi.

Hata hivyo, baadhi ya vituo vya televisheni vinavyotoa elimu au vya dini kama vile Mlimani TV, SUA ambao wamependekeza kuwapo na kundi maalumu la vituo ambavyo havitalipia gharama hizo kutokana wao kutoa huduma zaidi na si biashara.

Naye Mary Msuya wa Baraza la Wateja wa Huduma za Mawasiliano la TCRA, alisema pamoja na hoja za wadau za kuwa gharama za utangazaji kuwa juu, alitaka wananchi wa kawaida waendelee kupata matangazo bure husani kwa vituo vitano vyenye leseni ya kitaifa.

Awali, Mwenyekiti wa Jopo la Uchunguzi la TCRA, Jaji mstaafu Eusebia Munuo alisema kabla ya kuwasikiliza wadau wa utangazaji, umefanyika utafiti wa kuangalia gharama za urushaji wa vipindi vya televisheni kwa kuangalia gharama zenye ufanisi, zinazotambulika na zisizoumiza upande wowote.

“Tulishapata maoni tulipotembelea kampuni yanatorusha matangazo (wenye ving’amuzi) na hata vituo vya utangazaji baadhi waliotoa maoni yao kimaandishi, lakini leo tumetoa nafasi ya kusikiliza maoni zaidi,” alisema Jaji Munuo.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Utangazaji wa TCRA, Andrew Kisaka alisema lengo ni kuhakikisha pande hizo mbili zinatoa mapendekezo ya ada ya kurusha vipindi huku mwananchi akipata matangazo moja kwa moja bila kulipia.

 

Kampuni za simu zinazotoa huduma ya fedha kwa njia ya simu za mkononi katika kipindi cha miezi miwili iliyopita Novemba na Desemba mwaka jana zimekusanya kiasi cha Sh. trilioni 13.07.
Kaimu Meneja wa Habari Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Semu Mwakyanjala amesema kuna ongezeko kubwa la matumizi ya huduma za kifedha kwa njia ya mtandao hapa nchini.

Amesema kuwa katika miezi miwili iliyopita mwaka jana ambapo Novemba walikusanya Sh.trilioni 6.47 na Desemba Sh.trilioni 6.60 jumla ya makusanyo yote ni sh. Trilioni 13.07 kuptia kampuni za simu zinazohusika na huduma ya miamala.

Alitaja kampuni zilizohusika na maiamala hiyo ni pamoja na Zantel(Easy Pesa),Tigo (Tigo pesa), Vodacom(Mpesa), Aiterl(Airtel Money na Halotel (Halopesa).

Aidha aliwataka wananchi kujihadhari na utapeli unaofanywa kwa kutumia simu za mkononi huku mamlaka na vyombo vya usalama vinashughulikia suala hilo.

 

Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, unaosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), utaanza rasmi kutekelezwa mwezi ujao, imefahamika.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo mjini Dodoma wakati akijibu hoja za wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, waliokutana na watendaji wa wizara hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo, Profesa Muhongo ameongeza kuwa katika utekelezaji wa mradi huo, serikali imepanga kuwakabidhi makandarasi watakaotekeleza mradi huo kwa wabunge ili kuhakikisha kwamba mradi husika unatekelezwa kikamilifu.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2016/17 bungeni mwaka jana, Profesa Muhongo alisema serikali itafanya tathimini ya kina ya awamu ya kwanza na ya pili ya kupeleka umeme vijijini, lengo likiwa ni kuboresha maandalizi ya utekelezaji wa awamu ya tatu ya mradi huo.

Alisema pamoja na tathimini hiyo, masuala yatakayozingatiwa katika awamu ya tatu ni kupeleka umeme kwenye vijiji ambavyo havikupata umeme katika awamu ya kwanza na ya pili; kwenye viwanda vidogo vya uzalishaji mali; na katika shule za sekondari, hospitali, zahanati, vituo vya afya, pampu za maji na maeneo mengine muhimu ya huduma za kijamii.

Alisema awamu hiyo ya tatu, itaanza katika mwaka 2016/17 na kukamilika mwaka 2018/19.

Vijiji 8,000 vinatarajiwa kupatiwa umeme chini ya mradi wa REA Awamu ya Tatu. Wakati huo huo, Kamati hiyo ya Bunge kupitia kwa Mwenyekiti wake, Dotto Biteko imeipongeza Wizara ya Nishati na Madini kwa ukusanyaji wa maduhuli kwa kipindi cha nusu mwaka na kueleza kuwa mwelekeo wa ukusanyaji huo, unakwenda vizuri.

Awali, akiwasilisha taarifa ya wizara kuhusu upatikanaji wa fedha na utekelezaji wa majukumu kwa kipindi cha nusu mwaka kwa Kamati, Katibu Mkuu wa wizara, Profesa Justin Ntalikwa alieleza kuwa hadi kufikia Desemba 31 mwaka jana, wizara ilikuwa imekusanya jumla ya Sh bilioni 201.86 sawa na asilimia 54.46 ya lengo lililokusudiwa.

Chama cha Mapinduzi kimewashukuru watanzania kwa kukipa ushindi mkubwa katika chaguzi ndogo za madiwani na ubunge zilizofanyika mwishoni mwa wiki huku kikiweka hadharani siri ya ushindi.

Akizungumza na vyombo vya habari katika ofisi ndogo za makao makuu ya CCM Lumumba Dar es Salaam,  Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho Humprey Polepole amesema ushindi huo ni ishara tosha ya jinsi ambavyo watanzania wana imani na chama hicho, na kwamba kuna siri mbili kubwa zilizokipa chama hicho ushindi.

Siri ya kwanza aliyoitaja Polepole ni mageuzi ambapo uamuzi wa CCM kuzaliwa upya na kufanya mageuzi makubwa yanayolenga kukirudisha chama hicho kwa wanachama pamoja na kushughulika na shida na kero za watu umefanya watanzania wakielewe zaidi chama hicho.

Siri ya pili ya ushindi wa chama hicho kwa mujibu wa Polepole ni kazi nzuri ya serikali ya awamu ya tano                chini ya Rais Magufuli ambaye tangu apewe dhamana ya kuiongoza Tanzania ametekeleza kwa kiasi kikubwa ahadi nyingi nyingi alizoahidi ikiwemo ya kupambana na rushwa na ufisadi ikiwa ndiyo kazi ya kwanza aliyoanza nayo.

Polepole ametaja ahadi nyingine ambazo zimekuwa ni kivutio kikubwa na kuwafanya watanzania wakipe ushindi chama hicho ni utoaji wa elimu bure, ujenzi wa viwanda, miundombinu ikiwemo ununuzi wa ndege na zaidi ya yote kuwasikiliza wananchi na kero zao.

“Ushindi mliotupatia umetuimarisha kama chama licha ya hujuma, upotoshwaji mkubwa unaofanywa na vyama visivyokuwa CCM…. kubeza jina na nafasi ya Urais watanzania hawakuyaona hayo” Amesema Polepole

Polepole amesema chama hicho kinaendelea na mageuzi ya kiuongozi ili kukifanya kiweze kurudi kwenye misingi yake kwa kuwa na viongoz waadilifu, na wachapakazi, huku kikiendelea kutoa maelekezo kwa serikali kuhusu kuwatumikia wananchi jambo ambalo anaamini kuwa litafanya watanzania waendelelee kukipenda licha ya kubezwa na vyama visivyo kuwa CCM.

Katika chaguzi hizo, CCM imeshinda kwenye kata 19 kati ya kata 20 nchi nzima pamoja na kushinda ubunge katika jimbo la Dimani Zanzibar.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa tahadhari kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano juu ya utapeli unaofanywa kwa kutumia simu za mkononi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Meneja wa Mawasiliano kwa Umma wa TCRA, Semu Mwakyanjala alisema kumekuwa na ongezeko la matapeli wanaoghushi utaratibu wa mawasiliano na kuwalaghai watu kutuma pesa kwa simu za mkononi.

Mwakyanyala alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya huduma za kifedha na kwa miezi miwili iliyopita ya Novemba na Desemba, 2016 kwa wastani kiasi cha jumla ya fedha iliyopita katika mitandao ya kampuni zinazotoa huduma za kifedha kwa njia ya simu za mikononi ni Sh trilioni 13.07.

Aliongeza kuwa ni vyema wananchi wakazingatia mambo mbalimbali kabla ya kutuma fedha, ikiwemo kutokutekeleza maagizo yoyote yanayohusu fedha kwa mawasiliano ya simu hata kama yanatoka kwenye namba ya mtu anayemfahamu badala yake ampigie aliyemtumia ujumbe kwa namba nyingine kufanya uhakiki.

Pia aliwataka wananchi pale wanapopokea taarifa kwa njia ya simu au ujumbe mfupi wa maandishi kuwa ametumiwa fedha kwa makosa na kufuatiwa na kutumiwa ujumbe mfupi unaofanana na ujumbe unaotumwa na watoa huduma na kutakiwa kurudisha fedha hizo, asifanye haraka badala yake wachukue tahadhari zote kujiridhisha na uhalali wa taarifa hiyo.

“Omba taarifa fupi ya akaunti yako kwa mtoa huduma uhakiki miamala yako na salio lako ikibidi wasiliana na kituo cha huduma kwa wateja cha mtoa huduma wako kwa kuwa kumekuwepo na uhalifu wa kulaghai watoa huduma za mawasiliano kwa kutumia ujumbe mfupi unaokaribia kufanana na ujumbe unaotumwa na watoa huduma,” alieleza.

 

Walimu watatu mkoani Mwanza wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa kosa la  kukimbia vituo vyao vya kazi na kufanya kazi shule binafsi huku wakiendelea kupokea mishahara ya serikali

Taarifa ya jeshi la polisi mkoa wa Mwanza imewataja walimu hao waliokamatwa leo asubuhi katika mtaa wa Buhongwa wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza,kuwa ni pamoja na Richard Mgendi (30), Rwiza Ntare (27) na Gilbert Makwaya (33).

Walimu hao kila mmoja ana story yake kama ifuatavyo:-

Mwalimu Richard Mgendi alikuwa akifundisha shule ya sekondari ya Misasi wilayani Misungwi, mwaka 2012 alimuaga mkurugenzi wa wilaya hiyo kuwa anakwenda kusoma Mastersters ya lugha (Linguistic) katika chuo kikuu cha Mtakatifu Augustino, kwa kipindi chote hicho inadaiwa mwalimu huyo alikwenda kusoma na alipomaliza hakurudi katika shule yake ya awali bali alikuwa akifundisha shule binafsi ya sekondari iitwayo Musabe iliyopo Buhongwa huku akiendelea kulipwa mshahara kutoka serikalini.

Mwalimu Rwiza Ntare alikuwa akifundisha shule ya sekondari iitwayo Kigongo sekondari iliyopo wilaya ya Chato mkoani Geita ambapo mwaka 2015, alimuaga mkurugenzi wake kuwa anakwenda hospitali ya rufaa ya Bugando kupatiwa matibabu ya macho na vidonda vya tumbo lakini hakurudi tena bali inadaiwa alikuwa akifundisha shule binafsi ya sekondari iitwayo Musabe iliyopo mtaa wa Buhongwa huku akiendelea kulipwa mshahara na serikali.

Mwalimu Gilbert Makwaya alikuwa akifundisha Runima sekondari iliyopo maeneo ya Buhongwa na alimuaga mkurugenzi wa wilaya ya Nyamagana tarehe 27/09/2015 kuwa anakwenda kusoma Masters ya Hesabu katika chuo kikuu cha Mwenge kilichpo mjini Moshi lakini hakwenda bali alikuwa akifundisha shule binafsi ya Musabe iliyopo mtaa wa Buhongwa huku akiendelea kupokea mshahara kutoka serikalini.

Walimu wote watatu wapo katika mahojiano na jeshi la polisi na pindi uchunguzi ukikamilika watafikishwa mahakamani, jeshi la polisi linaendelea kuwatafuta baadhi ya walimu ambao wametoroka lakini inadaiwa wapo katika shule hiyo binafsi ya Musabe huku wakiendelea kulipwa mshahara na serikali pamoja na mkurugenzi wa shule hiyo.

Chanzo: eatv.tv

Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo amemshangaa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kwa kuendelea kung’ang’ania siasa hadi sasa hivi, badala yake anastahili kukaa kimya kula maisha ili afaidi uzee wake vizuri.

Bulembo aliyasema hayo wakati akifunga kampeni za udiwani Kata ya Mateves iliyopo Wilaya ya Arusha juzi, ambako walitarajiwa kumchagua diwani wao katika uchaguzi mdogo. Mbunge huyo mteule wa kuteuliwa, alisema anashangaa Lowassa kung’ang’ania madaraka, badala yake anastahili kula maisha ili kufaidi uzee wake vizuri.

Alisema wapinzani wataruhusiwa kutumia barabara, maji, shule na vinginevyo, lakini kwenda Ikulu haiwezekani. Aidha, Bulembo alilaani kitendo cha wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuingilia msafara wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliokuwa ukielekea Uwanja wa Ngorbob Sokoni kwa ajili ya kufunga kampeni za chama hicho.

Alisema wafuasi wa CCM ni wastaarabu na wavumilivu, hawakufanya fujo, bali waliwapita kwa mbele na kuelekea kwenye mkutano wa kufunga kampeni.

Mgombea Udiwani wa Kata ya Mateves, Julius Saing’ore maarufu kwa jina la Sovoyo na mgombea uenyekiti wa serikali ya kijiji, Mohamed Nassoro maarufu kwa jina la Arsenal, waliomba kura kwa wananchi hao ili walete maendeleo.

Mgombea udiwani Saing’ore aliwasihi wananchi wa kata hiyo, kumpa kura ili waliokwenda mahakamani kudai uchaguzi uliokuwa na kasoro wajue kuwa CCM ndio yenyewe.

Awali, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Shabani Mdoe alisema wananchi wana imani kubwa na chama hicho na hawataki porojo, bali wanataka maendeleo.

Alisisitiza kuwa awali alipokuwa madarakani aliyekuwa diwani wa CCM kabla ya kutenguliwa na mahakama mwaka jana, Saing’ore maarufu kwa jina la Sovoyo, alifanya kazi mbalimbali za maendeleo ikiwemo kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama.

Alisema diwani huyo ambaye sasa anagombea tena, alikaa madarakani kwa siku 63 kama Diwani wa Kata ya Mateves kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Arusha Vijiji (Arusha DC) hivyo kurudi kwake kama diwani kutawezesha wananchi kupata maendeleo.

Chanzo: Habari Leo

Mshauri maalumu wa Rais wa Gambia Adama Barrow amesema zaidi ya dola za Kimarekani milioni 11 zinaaminika kutoweka katika hazina ya serikali, kufuatia kuondoka madarakani kwa mtawala wa muda mrefu Yahya Jammeh.

Mia Ahmad Fatty amewaambia Waandishi wa habari katika mji mkuu wa Senegal Dakar kwamba wataalamu wa masuala ya fedha wanatathmini kujua ni kiasi gani kwa sasa kimepotea.

Amesema Gambia kwa sasa ina tatizo kubwa kifedha kwa hazina yake kutokuwa na kitu.

Kwa sasa Rais Barrow amekuwa akifanya kazi na timu ya wataalamu wa masuala ya fedha na wengine kutoka Benki kuu ya nchi hiyo kupata kiasi halisi kilichopo.

Habari zinasema magari ya kifahari na mali nyingine zilionekana zikipakiwa katika ndege ya mizigo ya Chad kwa niaba ya Rais Jammeh siku alipoondoka nchini humo.

Maelfu ya watu walikusanyika katika Ikulu ya nchi hiyo jana jioni wakiyaangalia majeshi ya Senegal yakiingia kwa ajili ya kuweka usalama kabla ya kurejea nchini kwa Adama Barrow.

Rais Barrow yupo nchini Senegal na bado haijulikani ni lini hasa atarudi Gambia na kuingia ofisini.

Alisema atarejea tu baada ya kuhakikishiwa usalama wake.

Serikali imewasilisha pendekezo la mabadiliko ya Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ili kuwezesha wanafunzi wanaochukua Stashahada katika vipaumbele vya kitaifa, kupewa mikopo ya kuwawezesha kuchukua elimu husika.

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alisema mabadiliko hayo, yamelenga kuwezesha kasi katika uchumi wa viwanda.

Profesa Ndalichako alisema mabadiliko katika Sheria Namba 4 ya Mwaka 2016 ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), yamelenga kutoa nafasi ya kada ya Stashahada inayohitajika ambao wamekuwa hawapati mikopo.

“Kwa lengo la kupata balance (mizania) na kwa kuwa Diploma nayo iko kwenye elimu ya juu, watoto ni wale wale. Kuna wengine nao wanashindwa kumudu gharama na ili serikali ipate uwiano mzuri tumeona ni vizuri kuwe na marekebisho ya sheria,” alieleza Profesa Ndalichako.

Profesa Ndalichako alisema kuna umuhimu mkubwa wa kada ya Stashahada, hasa wanaokwenda sanjari na vipaumbele vya kitaifa kwenye msukumo wa Serikali ya Awamu ya Tano wa ujenzi wa taifa la vijana, kama ilivyo kwa wenye Shahada.

“Kama taifa tunazungumzia uchumi wa viwanda,wadau wote hata wale wa ngazi ya kati ni muhimu katika kuhakikisha kwamba ajenda hii inafanikiwa kama vile ambavyo wale wa digrii wangelifanya,” aliongeza waziri huyo.

Mwaka 2004, kulikuwepo na mabadiliko katika sheria hiyo iliyowezesha wanaochukua masomo ya sayansi, hisabati na elimu ya msingi (kwenye msisitizo wa sayansi na hisabati), kupata mikopo ya elimu, nafasi iliyoanza kutumika mwaka 2014, lakini hatua hiyo ilisimamishwa wakati wa muhula wa masomo wa mwaka 2016/17.

Hata hivyo, HESLB ilikaririwa ikisema kwamba maamuzi ya kusitisha utoaji wa mikopo, ililenga kutekeleza maagizo ya serikali. Hata hivyo, jana Profesa Ndalichako alisema kwamba uamuzi wa kusimamisha mikopo hiyo,ulitokana na nia ya serikali kufanya mabadiliko katika sheria hiyo ili kuipa wigo mpana zaidi kuliko kujikita katika eneo la sayansi pekee.