Habarika | Kimataifa
layout-wrap boxed
Tuesday, May 22, 2018

Kimataifa

Rais wa Marekani Donald Trump amesema serikali yake itaanza mara moja kushughulikia ujenzi wa ukuta kati ya Marekani na Mexico ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake kubwa aliyoiweka wakati wa kampeni za uchaguzi.

Akizungumza na wafanyakazi wanaohusika na usalama wa taifa, Donald Trump amesema ukuta huo utazuia wahamiaji haramu na wafanyabiashara wa dawa za kulevya, kwa kuongeza kuwa siku zao zimekwisha wao kuishi na kufanya uharibifu.

Amesisitiza kauli yake ya kutaka Mexico kulipia ukuta huo, licha ya Mexico kukataa kufanya hivyo.

Wakati Marekani ikiweka msimamo wake huo, serikali na raia wa Mexico nao wameingilia kati kutetea nchi yao.

Rais wa Mexico Enrique Pena Nieto naye anashinikizwa kufuta mkutano wake na Rais Trump unaotarajiwa kufanyika wiki ijayo mjini Washngton, ikiwa kama ni kujibu uamuzi huo wa Marekani kujenga ukuta.

Meya wa mji wa Mexico City Miguel Espinosa amesema kujengwa kwa ukuta huo, Marekani itajitenga yenyewe sio tu na Mexico bali na Amerika ya kusini yote.

Wakati huohuo, Rais wa Marekani amesema kuwa ana amini kwamba njia ya mateso inayotumika kuwahoji washukiwa wa ugaidi inafanya kazi vilivyo.

Akihojiwa na kituo cha Televisheni cha ABC, amesema Marekani inapaswa kupambana kwa nguvu zote katika kujibu mateso yaliyofanywa na kundi la Islamic State kwenye eneo la mashariki ya kati.

Mtangulizi wake Rais Barack Obama alipiga marufuku njia hiyo ya kutumia maji kuwahoji washukiwa kutokana na kuleta mabishano, mbinu hiyo ilikuwa ikitumika wakati wa utawala wa George Bush.

Rais wa Marekani Donald Trump anatarajiwa kutia saini amri kuu kuweka masharti kuhusu wahamiaji wanaoingia nchini humo.

Taarifa kutoka Marekani zinasema ataanza kwa hatua ya kuimarisha usalama katika mpaka wa nchi hiyo na Mexico atakapozuru makao makuu ya wizara ya usalama wa ndani baadaye Jumatano.

Aidha, anatarajiwa pia kutoa tangazo la kuidhinisha sheria kali zaidi za kupata visa kwa wageni kutoka eneo la Mashariki ya Kati na Afrika ambayo yana Waislamu wengi.

Bw Trump ameandika kwenye Twitter kwamba leo itakuwa siku muhimu sana kwa usalama wa taifa la Marekani.

Mwandishi wa BBC David Willis kutoka Washington anasema hatua hiyo huenda ikayaudhi mashirika ya kibinadamu na yale ya kutoa misaada ikizingatiwa mzozo unaoendelea kwa sasa kuhusu hali ya wakimbizi wa Syria.

Wakati wa kampeni yake ya urais, Donald Trump aliahidi kufanyia mageuzi suala la uhamiaji Marekani.

Aligusia ujenzi wa ukuta kati ya Mexico na Marekani kuzuia wahamiaji haramu na kuwapiga marufuku Waislamu kuingia katika taifa hilo kama sehemu ya vita dhidi ya ugaidi. Baadaye alibadili msimamo kidogo na kufafanua kwamba watakachofanyiwa Waislamu ni kufanyiwa ukaguzi mkali kabla ya kuruhusiwa kuingia Marekani.

Anatarajiwa kufika katika wizara ya usalama wa ndani baadaye leo na anatarajiwa kusaini maagizo hayo ya kuimarisha usalama katika mpaka wa Mexico na taifa lake na baadaye wiki hiii taarifa zinaashiria atawajibikia ahadi yake ya kupunguza idadi ya wakimbizi wanaoingia Marekani.

Na hiyo ni hadi pale ukaguzi mkali utakapoanzishwa na kuzuia raia wa mataifa saba ya Afrika na kutoka eneo la Mashariki ya Kati yote yalio na idadi kubwa ya waumini wa Kiislamu.

Ubaguzi wa kidini unapigwa marufuku kwa mujibu wa katiba ya Marekani lakini inadhaniwa utawala wa Trump utaidhinisha marufuku hiyo kwa misingi kwamba ni hatua za dharura kukabiliana na tishio lililopo la ugaidi.

Awali, Bw Trump aliandika kwenye Twitter kueleza kusikitishwa kwake na kiwango cha juu cha ghasia na mauaji katika jiji la Chicago.

Vyombo vya habari wiki hii viliripoti kwamba tayari watu 228 wamepigwa risasi na wengine zaidi ya 40 kuuawa mwaka huu.

Bw Trump ameandika kwamba iwapo watawala wa Chicago hawatatua tatizo hilo la mauaji, basi atawatuma ‘Feds’ akimaanisha maafisa wa FBI.

 

Wanawake wanaojitoa mhanga nchini Nigeria wameanza kutumia watoto kuepuka vizuizi vya ukaguzi, jambo ambalo, serikali nchini humo inasema linaweza kuwa mwelekeo wa hatari.

Tahadhari hiyo imekuja baada ya wanawake wawili waliokuwa wamebeba watoto mgongoni kufanya mashambulizi ya kujitoa mhanga katika mji wa Madagali siku 10 zilizopita.

Januari 13 mwaka huu, wanawake wanne waliokuwa wakijitoa mhanga walifika kwenye mji wa Maddaggalee katika jimbo la Adamawa, wawili walitambuliwa na walinzi waliokuwa katika vizuizi na kutakiwa kusimama, baada ya mbinu zao kugundulika.

Lakini wengine wawili walifanikiwa kupita bila ya kugunduliwa. kubeba kwao watoto kulifanya wasigunduliwe na kuweza kusababisha maafa yaliyosababisha vifo vya watu wanne, wao wenyewe kufariki na watoto wawili pia waliokuwa wamewabeba katika mawili tofauti.

Kundi la Boko Haram linajulikana kwa kuwatumia wanawake, hususan wasichana katika mabomu ya kujitoa mhanga, Hata hivyo ni mara ya kwanza katika maasi hayo kutumia watoto wachanga.

 

Rais wa Marekani Donald Trump amefanya kile alichokiita siku yake ya kwanza kuanza kazi katika utawala wake, kutokana na uamuzi alioufanya wa nchi yake kujiondoa katika mpango wa Ushirikiano wa kiuchumi wa nchi zinazounganishwa na bahari ya Pasifiki ambapo pia ameonya pia kuyapa adhabu makampuni ya nchi hiyo yanayopeleka kazi nje ya nchi.

Makubaliano ya Mpango wa Ushirikianio wa Kibiashara wa nchi zinazounganishwa na Bahari ya Pacific TPP, yalijadiliwa na utawala wa Rais Barack Obama.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Sean Spicer anasema hatua hiyo ni dalili ya kuanza kwa enzi mpya ya sera za biashara za Marekani.

”Kama alivyokuwa akisema Rais mara nyingi, hii ni aina ya makubaliano ya mataifa mengi na si kwa maslahi mazuri kwetu, na amekua akienda haraka kuboresha sera za kibiashara ambazo zitaongeza ushindani wa wafanyakazi wa Marekani na uzalishaji…” Alisema Sean Spicer

Amesema amri hiyo ya Rais inaongoza katika enzi mpya ya sera za biashara ya Marekani, ambayo utawala wa Trump utapata fursa ya kufanya biashara na washirika wake duniani kote.

Lakini si hatua hiyo tu aliyoichukua Rais Trump, katika wiki yake ya kwanza ofisini, Rais Trump pia amerejesha amri ya kupiga marufuku utoaji wa fedha za serikali kwa makundi ya kimataifa ambayo yanazitumia katika kushughulikia ama kujadili utoaji mimba kama njia moja wapo ya uzazi wa mpango.

Uamuzi huo ni taarifa ya kwanza ya utawala mpya wa Marekani kutoa kuhusiana na misaada inayotoa kimataifa.

Utawala unaongozwa na chama cha Republican nchini Marekani mara zote umekuwa ukipiga marufuku msaada wa serikali kwa mashirika yasiyo ya kiserikali ya kimataifa ambayo yanatoa huduma za utoaji mimba.

Wakati huohuo Baraza la Senete nchini Marekani limemthibitisha Mike Pompeo kuwa mkurugenzi mpya wa Shirika la Ujasusi nchini humo CIA.

Waandishi wa habari wanasema kazi yake ya kwanza itakuwa kurejesha uhusiano mzuri katui ya shirika hilo na Rais Donald Trump, ambaye amekuwa akilikosoa kwa kile ilichosema kwamba Urusi ilimsaidia wakati wa uchaguzi

 

Shirika moja la kisheria nchini Marekani limetangaza kwamba litawasilisha kesi dhidi ya Rais Donald Trump.

Shirika hilo linamtuhumu kiongozi huyo kwa kikiuka marufuku iliyowekwa kwenye katiba dhidi ya kupokea malipo kutoka kwa serikali za nchi za nje.

Kundi la mawakili na watafiti linasema Bw Trump amekuwa akipokea malipo kutoka kwa serikali za nje kupitia wageni kwenye hoteli zake na majumba yake ya kukodisha.

Wanasema kuna kifungu kwenye sheria ya nchi hiyo ambacho kinaharamisha malipo kama hayo.

Mwanawe Donald Trump, Eric, ametaja hatua hiyo kama “usumbufu tu kwa nia ya kujifaidisha kisiasa”.

Eric Trump, ambaye ni makamu rais mtendaji wa shirika la Trump Organization ambalo linamiliki na kusimamia biashara za rais huyo, amesema kampuni hiyo imechukua hatua kubwa kufuata sheria kuzuia kesi, kwa mujibu wa New York Times.

Amesema kampuni hiyo imeahidi kutoa faida kutoka kwa hoteli zake ambazo zimetokana na wageni kutoka serikali za nje na kuziwasilisha kwa Hazina Kuu ya Marekani.

‘Tumelazimishwa kuchukua hatua’

Shirika hilo la Citizens for Responsibility and Ethics in Washington (Crew) limesema litawasilisha kesi katika mahakama ya Manhattan, New York Jumatatu asubuhi.

“Hatukutaka kufika hapa,” mkurugenzi mkuu mtendaji Noah Bookbinder alisema kupitia taarifa.

“Matumaini yetu yalikuwa kwamba Rais Trump angechukua hatua zifaazo kuzuia kukiuka Katiba kabla yake kuingia madarakani. Tumelazimishwa kuchukua hatua za kisheria.”

Katiba ya Marekani inasema hakuna afisa yeyote wa serikali anayefaa kupokea zawadi au “malipo yoyoye ya kifedha, au ada kutoka kwa serikali ya kigeni.

Mawakili wa Bw Trump wanadai sheria hiyo ni ya kutumiwa tu kuzuia maafisa wa serikali kupokea zawadi au manufaa maalum kutoka kwa nchi za nje na wala si kwa malipo kama vile bili ya hoteli.

 

Viongozi wa nchi za Afrika Magharibi wamempa Yahya Jammeh fursa ya mwisho kuachia madaraka, huku wanajeshi wa Senegal wakiingia nchini Gambia.

Bw Jammeh amepewa hadi saa sita mchana Ijumaa kuachia madaraka la sivyo aondolewe kwa nguvu na wanajeshi wa nchi za Afrika Magharibi wanaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ambapo wanajeshi hao wametakiwa kusubiri hadi muda wa fursa ya mwisho aliyopewa utakapomalizika

Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi (Ecowas) inamuunga mkono Adama Barrow, ambaye aliapishwa kuwa rais mpya wa Gambia katika ubalozi wa nchini hiyo nchini Senegal.

Juhudi za mwisho za kumshawishi Bw Jammeh kuondoka kwa hiari, ambazo zinaongozwa na Rais wa Guinea Alpha Conde, zinatarajiwa kufanyika Ijumaa asubuhi.

Mwenyekiti wa tume ya Ecowas, Marcel Alain de Souza, alisema iwapo mkutano huo utakaoongozwa na Bw Conde hautafaulu, basi hatua ya kijeshi itafuata.

“Iwapo kufikia saa sita mchana, yeye (Bw Jammeh) hatakubali kuondoka Gambia chini ya Rais Conde, tutaingilia kijeshi,” amesema.

Wanajeshi kutoka Senegal na nchi nyingine za Afrika Magharibi waliingia Gambia baada ya muda wa nafasi za mwisho alizopewa Bw Jammeh kuondoka kumalizika.

Bw Jammeh, ambaye bado yupo nchini Senegal amesema hatarejea mji mkuu wa Gambia, Banjul, hadi operesheni ya kijeshi imalizike.

Hatua ya Ecowas kutaka kumtoa kwa nguvu Jammeh inaungwa mkono na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 15, ingawa baraza hilo lilisisitiza kwamba suluhu ya amani inafaa kutopewa kipaumbele.

Katika hali isiyo ya kawaida mbunge mmoja nchini Kenya amewakataza wanawake wa nchi hiyo kukutana kimwili na waume zao ili kuwabana kwenda kujiandikisha katika daftari la uchaguzi mkuu.

Mbunge huyo wa Mombasa, Misho Mboko amesema njia pekee ya kuwabana wanaume kwenda kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Kenya utakaofanyika mwezi Agosti ni kukataa kushiriki tendo la ndoa hadi wawaonyeshe vitambulisho vya kupigia kura.

“Wanawake hii ni mbinu ambayo mnatakiwa kuitumia, ni njia nzuri. Mkatae kufanya nao mapenzi hadi wawaonyeshe kadi zao za kupigia kura,” alisema Mboko.

Mboko ametumia mbinu hiyo ili wanaume wengi wajitokeze kupiga kura kwa kujiandikisha mapema na kupata vitambulisho kabla ya zoezi la kuandikisha wapiga kura kufungwa Februari, 17.

Vyombo vya habari nchini Marekani vimesema kuwa aliyekuwa rais wa taifa hilo George Bush anapata matibabu katika hispitali moja ya Houston katika jimbo la texas.

Maelezo kuhusu hali yake hayajatolewa ,lakini mkuu wa wafanyikazi wake amenukuliwa akisema kuwa bw Bush aliye na umri wa miaka 92 yuko katika hali nzuri na kwamba huenda akatolewa na kwenda nyumbani katika siku chache zijazo.

Bush kama marais wengine wa zamani anatarajiwa kuhudhuria kuapishwa kwa rais mteule wa Marekani Donald Trump katika sherehe itakayofanyika siku ya Ijumaa.

Rais wa Urusi Vladimir Putin, amesema kuuawa kwa balozi wa taifa lake nchini Uturuki Andrey Karlov siku ya Jumatatu ni uchokozi ambao lengo lake ni kuvuruga juhudi za kutafuta amani Syria.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, alisema kuuawa kwa balozi huyo ni shambulio dhidi ya taifa la uturuki.

Bw Karlov aliuawa kwa kupigwa risasi na afisa wa polisi ambaye hakuwa kwenye zamu, alipokuwa anatoa hotuba kwenye maonesho ya picha katika mji mkuu Ankara.

Picha za video zilimuonesha mshambuliaji, akiwa amevalia suti na tai, akimfyatulia risasi balozi huyo kutoka nyuma, akisema kwa sauti ujumbe kuhusu mji wa Aleppo, Syria ambapo pia mshambuliaji huyo aliuawa kwa kupigwa risais na polisi huku Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeshutumu mauaji hayo.

Taarifa zinasema muuaji ni Mevlut Mert Aydintas, 22, ambaye alikuwa anahudumu katika kikosi cha polisi kupambana na fujo mjini Ankara ambapo haijabainika iwapo ana uhusiano wowote na kundi lolote.

Tukio hilo lilitokea siku moja baada ya maandamano kufanyika Uturuki kupinga hatua ya Urusi kumuunga mkono Rais wa Syria Bashar al-Assad.

Recep Tayyip Erdogan alizungumza na Bw Putin kwa njia ya simu, na kwenye ujumbe wa video, alisema wote wawili walikubaliana kisa hicho kilikuwa “uchokozi”.

Alisema wale waliotaka kuharibu uhusiano baina ya nchi hizo mbili hawatafanikiwa.

Bw Putin kwa upande wake alisema “bila shaka ni kisa cha uchokozi chenye lengo la kuvuruga kurejea hali ya kawaida” kwa uhusiano wa kidiplomasia na “shughuli ya kutafuta amani Syria”

Wachunguzi kutoka Urusi wametumwa Uturuki kuchunguza kisa hicho, msemaji wa Bw Putin, Dmitry Peskov amesema.

Katibu Muu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon na Rais wa Ufaransa Francois Hollande amelaani mauaji hayo. Mawaziri wa Marekani, Uingereza, Ujerumani pia wameshutumu mauaji hayo.

Kundi linaloongozwa na kiongozi wa kidini aliyetorokea Marekani Fethullah Gulen pia limeshutumu mauaji hayo na kujitenga na muuaji huyo.

Karlov, 62, ni mwanabalozi wa muda mrefu wa Urusi.

ALihudumu kama balozi wa Muungano wa Usovieti nchini Korea Kaskazini miaka ya 1980.

Baada ya kuvunjika kwa muungano huo mwaka 1991, alihudumu kama balozi Korea Kusini kwa miaka kadha kabla ya kurejea Korea Kaskazini mwaka 2001.

Alitumwa Ankara Julai 2013.

Rais mteule nchini Marekani Donald Trump amethibitisha kuwa mkuu wa kampuni ya Exxon Mobil, Rex Tillerson ndiye waziri wa mambo ya nje nchini Marekani.

Bwana Trump alimsifu Tillerson mwenye umri wa miaka 64 kama mmoja wa viongozi wa biashara wenye tajriba kubwa zaidi duniani.

Bwana Tillerson anatajwa kuwa na uhusiano mwema na rais wa Urusi Vladimir Putin jambo ambalo limewatia wasiwasi wa wanachama wa Democratic na baadhi ya wale wa Republican ambapo uteuzi huo unahitaji kuthibitishwa na bunge la Senate.

Siku chache zilizopita ilibainika kuwa majasusi nchini Marekani wanaamini kuwa Urusi ilihusika na kushawishi ushindi wa Trump.

Waziri wa mambo ya nje wa nchini Marekani ndiye mwanadiplomasia wa cheo cha juu zaidi ambaye uhusika na sera za kigeni za nchi.