Habarika | JELA MIAKA MIWILI KWA WATAKAOTUMIA VIELELEZO VYA TAIFA KUTANGAZA BIASHARA ZAO
layout-wrap boxed
Sunday, April 22, 2018

JELA MIAKA MIWILI KWA WATAKAOTUMIA VIELELEZO VYA TAIFA KUTANGAZA BIASHARA ZAO

Mpigachapa Mkuu wa Serikali, Cassian Chibogoyo ametoa onyo kwa watumiaji vibaya vielelezo vya Taifa ambavyo ni wimbo wa taifa, bendera pamoja na nembo ya serikali.

Amesema watakaotumia vielelezo hivyo kama alama za biashara yake au kutumika kwa matangazo ya biashara yake, kutumika kwa matangazo ya biashara au shughuli za kitaaluma au kwenye maandiko yanayokusudia mauzo au taaluma au kukashfu vielelezo hivyo anakabiliwa na kosa na adhabu yake ni kifungo cha miaka miwili jela.

Alisema bendera inatakiwa kupewa hadhi kwa kutoruhusiwa kupeperushwa bendera iliyopauka, kutoboka au chafu huku wananchi wakirudisha maadili ya kuheshimu bendera wakati wa kupandishwa au kushushwa.

Pia aliwataka wanaotumia nembo ya serikali pamoja na bendera ambazo siyo sahihi zilizotengenezwa na watu mbalimbali kuziondoa, kwani zipo bendera ambazo zimewekwa rangi ambayo siyo zinazotakiwa huku wengine wakiweka nembo iliyotengenezwa tofauti na matakwa ya serikali na wengine wakiimba wimbo wa taifa kwa kuweka vibwagizo mbalimbali.

Akizungumza jana kuhusu vielelezo hivyo, Chibogoyo alisema kwa sheria na kwa kuwa nchi inaongozwa kwa utawala wa sheria hairuhusiwi mtu kuweka nembo hizo katika nguo labda kama itatakiwa kufanyiwa maboresho kwa ajili ya uzalendo.

Alisema kwa mujibu wa sheria ya nembo ya taifa ya mwaka 1971 bendera ya taifa inapaswa kuwa na rangi ya bluu, njano, nyeusi na kijani huku kukiwa na muundo wa uwiano wa urefu kwa upana ni futi mbili kwa tatu au futi sita kwa nne.

Alisema katika matumizi ni rais pekee ndiyo anaweza kufanya mabadiliko kwa mujibu wa sheria hivyo anayebadilisha kwa namna yoyote atachukuliwa hatua za kisheria.

Alisema bendera ndogo zinatakiwa kutumiwa katika shughuli za kimataifa na kitaifa pamoja na bendera ya rais ikitumika wakati rais akiwepo huku zikikaa upande wa kulia katika magari ya Rais, Makamu wa Rais, na Waziri Mkuu. Spika na jaji ikikaa upande wa kushoto wa gari na kupepea popote alipo.

Alisema kwa mawaziri na manaibu waziri bendera zinapepea upande wa kushoto katika mikoa yote isipokuwa mikoa ya Dodoma na Dar es Salaam huku wakuu wa mikoa na wilaya wakipeperusha bendera wakiwa mikoani na wilayani mwao tu.

Akizungumzia wimbo wa taifa alisema ni dua pekee la nchi linalomtaja Mungu na kuamini katika Mungu na inatakiwa kuimbwa katika mikusanyiko mikubwa ya kuwakilisha Taifa au timu ya taifa au nyingine inayowakilisha nchi na shuleni.

Sambaza Makala hii: Share on Facebook0Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn0Share on Google+0Email this to someone

You may also like

0 comments

By