Habarika | HOTUBA YA MUSEVENI YAWACHEFUA MABALOZI KUTOKA MAGHARIBI
layout-wrap boxed
Sunday, April 22, 2018

HOTUBA YA MUSEVENI YAWACHEFUA MABALOZI KUTOKA MAGHARIBI

Mabalozi kutoka nchi za Magharibi waliondoka kwa hasira kutoka kwenye sherehe ya kuapishwa kwa Rais Yoweri Museveni hapo jana

Mabalozi hao kutoka Marekani, nchi za Ulaya na Canada waliondoka ghafla baada ya Bw Museveni kushutumu vikali Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC).

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema mabalozi hao pia walikerwa na kuwepo kwa Rais wa Sudan Omar al-Bashir kwenye sherehe hiyo ambaye anasakwa na mahakama ya ICC kwa tuhuma za kuhusika katika mauaji ya halaiki.

Sherehe hiyo ya kuapishwa kwa Bw Museveni, ya tano tangu achukue madaraka mwaka 1986, ilihudhuriwa na viongozi kutoka Chad, Ethiopia, Kenya, Somalia, South Africa, South Sudan, Tanzania na Zimbabwe

Akihutubu, Bw Museveni alisema ICC ni “kundi la watu bure” na akasema haiungi mkono tena.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Elizabeth Trudeau alisema: “Kutokana na kuwepo kwa Rais Bashir na matamshi ya Rais Museveni, ujumbe wa Marekani, pamoja na wawakilishi kutoka nchi za EU na Canada, waliondoka kutoka kwenye sherehe kuonyesha kutofurahishwa kwao (na vitendo hivyo).”

“Tunaamini kwamba kuondoka kwenye sherehe ndilo jibu sahihi kwa kiongozi wa nchi anayepuuzilia mbali juhudi za kuhakikisha haki kwa waathiriwa wa mauaji ya halaiki, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.”

Bi Trudeau alisema inashangaza zaidi ikizingatiwa kwamba Uganda ni taifa mwanachama wa Mkataba wa Roma, mkataba uliounda mahakama ya ICC.

Mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi ilitoa vibali vya kukamatwa kwa Bw Bashir mwaka 2009 na 2010 kwa makosa ya mauaji ya halaiki yanayodaiwa kutekelezwa eneo la Darfur, magharibi mwa Sudan.

Sambaza Makala hii: Share on Facebook5Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn0Share on Google+0Email this to someone

You may also like

0 comments

By