Habarika | FAINI YA KUTOVAA HELMET KWENYE BODABODA SASA NI SH. 300,000/=
layout-wrap boxed
Friday, April 27, 2018

FAINI YA KUTOVAA HELMET KWENYE BODABODA SASA NI SH. 300,000/=

Biashara ya Bodaboda imeshamiri katika Jiji la Dar es Salaam lenye wakazi zaidi ya milioni nne. Hata hivyo, licha ya ukweli kwamba helmeti kupunguza kwa asilimia 69 hatari ya mwendesha pikipiki kuumia kichwa pale apatapo ajali, na kapunguza kifo kwa asilimia 42, uvaaji wa helmeti kwa madereva na abiria wao bado ni kitendawili.

Kamanda wa Usalama Barabarani Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Awadhi Haji anasema wameshatoa elimu ya kutosha kwa waendesha pikipiki ili wahakikishe wanavaa kofia ngumu pamoja na abiria wao wakati wanapopanda pikipiki.

“Watakaokaidi agizo tutawakamata madereva na abiria wao na kuwafikisha mahakamani. Huko wanaweza kutozwa faini inayoanzia Sh 300,000 au kufungwa jela kati ya miezi sita au mwaka mmoja kutokana na sheria ya Sumatra,” anasema kamanda Haji.

Polisi wameamua kufanya hivyo kutokana na faini ya Sh 30,000 chini ya sheria ya usalama barabarani kutowaogopesha madereva wengi wa pikipiki. Ndiyo maana sasa uamuzi ni kuwapeleka mahakamani.

“Huko tunawashitaki chini ya sheria ya Sumatra na operesheni hii tunaifanya kwa kushirikiana na Sumatra wenyewe,” anasema ACP Haji.

Gasper Athony wa Chuo cha Future World kinachotoa mafunzo kwa madereva wa pikipiki kwa kushirikiana na Chuo cha Mafunzo Stadi (Veta), anasema zimethibitisha kwamba wapanda pikipiki wasiovaa helmeti wanapoanguka wanaumia zaidi kuliko wale waliovaa helmeti.

“Idadi ya waliojeruhiwa kichwani wakati wamevaa helmeti ni ndogo ukilinganisha na idadi ya watu waliojeruhiwa kichwani wakiwa hawakuvaa helmeti. Kofia hizi ni muhimu kwa dereva na abiria wa Bodaboda,” anasema Antony.

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2015 inaielezea Tanzania kwamba usimamizi wa vihatarishi vya uvaaji wa helmeti hapa nchini unatekelezwa alama 4 kati ya alama 10.

Hii maana yake ni kwamba Mamlaka zinazosimamia usafiri hapa nchini hususan Jeshi la Polisi na Sumatra zinatekeleza kwa kiwango cha chini katika kuhakikisha sheria zinafuatwa na waendesha Bodaboda linapokuja suala la uvaaji wa helmeti.

Kwa mujibu wa Antony, ambaye ni mkufunzi wa madereva wa Bodaboda, uvaaji wa helmeti unapunguza kujeruhiwa kichwani mara tatu.

“Sehemu ngumu ya nje inazuia kupenya kwa kitu chochote na sehemu ya ndani ya kofia hiyo inasaidia kupunguza mgandamizo. Hali kadhalika, helmeti nyingi zina sehemu ya kukinga macho dhidi ya vumbi, upepo na kuzuia wadudu wanaoruka, hivyo dereva kuendesha pikipiki bila kuvaa helmeti anaweka maisha yake na ya abiria katika hatari kubwa,” anasisitiza Antony.

Kuna aina nne za helmeti na ya kwanza ni Full Face ambayo inafunika uso wote, pili ni aina ya Motor Cross ambayo nayo inafunika kichwa chote pamoja kidevu.

Aina ya tatu ni Modula ambayo inafunika kichwa; lakini inakuwa na kioo cha kufunua na ya mwisho ni Open Face ambayo inafunika kichwa lakini haina kioo mbele.

Robert Mnyambe, mmoja wa madereva wa bodaboda mjini Morogoro, anakiri kwamba madereva wengi wa pikipiki hawapendi kuvaa helmeti kwa madai kwamba uvaaji wa kofia hiyo ngumu unapunguza uwezo wa kuona na kusikia vizuri hivyo kusababisha ajali nyingi.

Kwa upande wa abiria, Mnyambe anasema wengi wa abiria; hasa wanawake hawataki kuvaa helmeti kwa sababu mbalimbali.

Kuna madai ya kuogopa kuchangiana jasho kwa vile zinavaliwa na abiria wengi. Kubwa zaidi ya madai ya abiria wanawake ni eti kwamba helmeti zinavuruga nywele zao ambazo wanatumia gharama kubwa kuzitengeneza.

Mfano mzuri ni Neema Wema mkazi wa Dar es Salaam, yeye hukataa kuvaa helmeti eti kwa kuwa anahofia kuambukizwa magonjwa ya ngozi kutokana na kofia hizo kutumiwa na abiria walio wengi.

“Kofia za hawa bodaboda hawazifanyii usafi. Zinanuka. Ndio maana sivai,” anasema Neema na kuongeza, “Dar es Salaam ni joto kali, ukiivaa kofia hii lazima tu utaivua maana inaleta joto na hiyo kuwa na harufu kali.”

Dereva mwingine wa bodaboda, James Kemege, na ambaye anafanya biashara hiyo kwa mwaka wa tatu sasa anasema: “Mimi nina helmeti mbili ya kwangu na abiria. Lakini abiria wengi hawataki kuvaa helmeti hasa wanawake kwa madai kuwa nywele zao zinaharibika pia wanadai zina uchafu.”

Kemege anasema abiria wake wanadai helmeti zinaambukiza ugonjwa wa ngozi, mba. Anaasema wanadai wanaogopa kuambukizwa magonjwa ya ngozi kutokana na kofia hiyo kuvaliwa na watu wengi. Kwa mawazo yake Kemege, serikali iwachukulie hatua abiria wanaokataa kuvaa helmeti ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani.

“Sisi madereva tukikosea tunapelekwa mahakamani. Iwe vivyo hivyo pia kwa abiria. Na watozwe Sh 50,000 wanapokutwa na hatia sawa na dereva.”

Lakini, Anneth Mwakajumba anasema abiria wengi hawavai kofia ngumu kwa sababu hakuna ufuatiliaji kutoka kwa polisi jambo ambalo abiria wanaona sio jambo la lazima kuvaa hiyo kofia.

“Sijawahi kuona polisi inamkamata mwendesha bodaboda ambaye hajavaa helmeti au abiria aliyekamatwa kwa kupanda bodaboda bila kuvaa helmeti. Kwa kuwa hakuna ufuatiliaji ndio maana watu wengi wanapuuzia kuzivaa, lakini polisi wakikomaa abiria tutavaa tu kwa lazima maana ni kwa manufaa ya maisha yetu,” anasema Anneth.

Dk Mariam Kalomo, wa Kitengo cha Tiba, Wizara ya Afya, anaeleza kofia ngumu zinapovaliwa na abiria mbalimbali zinaweza kuambukiza magonjwa ya ngozi kama malengelenge, fungasi na seabies.

“Sisi madaktari tunawashauri wateja wa bodaboda wawe na tabia ya kununua kofia zao kama hawataki kuambukizwa hayo magonjwa. Lakini pia ni afadhali maambukizi kwa kuwa yanatibika kuliko upate ajali ambayo inapelekea kifo,” anasema Dk Kalomo.

Hata hivyo, hakuna takwimu za watu waliougua magonjwa ya ngozi kwa kuvaa helmeti. Mkurugenzi wa Global Helmet Vaccine Initiative (GHVI), Alpherio Nchimbi, anasema utafiti uliofanywa na na taasisi yake katika mikoa ya Tanga, Morogoro na Dar es Salaam unaonesha kuwa wanaume wengi wanavaa helmeti kuliko wanawake.

“Wanaume wanaovaa helmeti ni zaidi ya mara nne ya wanawake, hii inadhihirisha kwamba wanawake hawapendi kuvaa kofia ngumu na hata akipewa na dereva yuko radhi kuishikilia mkononi,” anabainisha Nchimbi. Anashauri kwamba wateja wa bodaboda wapewe elimu ili kila mtu anunue kofia ngumu na kukaa nayo ndani.

“Kila nyumba ina mwavuli licha ya kuwa sio wakati wote mvua zinanyesha. Ifikie wakati kila nyumba iwe na kofia ngumu ili siku itakapolazimu kupanda pikipiki atumie ya kwake.”

Wazo hili linaungwa mkono na abiria Flora Kamage, kwamba abiria wanaoutumia zaidi usafiri wa pikipiki waone umuhimu wa kununua kofia zao. Hii ni itasaidia kujikinga na uchafu na magonjwa ya ngozi kwa kutumia kofia inayotumiwa na watu wengi.

Ofisa Mfawidhi wa Sumatra mkoani Iringa, Patel Ngereza, anasema dereva wa bodaboda atatakiwa kuvaa kofia kwa ajili ya usalama wake na abiria. Kwa maelezo ya Ngereza, sheria ya ulipaji wa leseni ya bodaboda iliyopitishwa na Bunge mwaka 2011, inapaswa kutumika ipasavyo, ili kuzuia ajali zinazosababishwa uzembe wa madereva.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoani Iringa, Leopold Fungu , anasema polisi wa kikosi hicho wamekuwa wakiwakamata na wataendelea kuwakamata madereva wa Bodaboda na wengine ambao hawazingatii sheria za usalama barabarani na sheria nyingine za nchi.

Fungu anasema madereva wengi wa bodaboda wamekuwa wakikamatwa kwa makosa makubwa saba ambayo ni pamoja na kuendesha chombo hicho bila kuwa na leseni, wakiwa wamelewa, hawajavaa helmeti, wamevaa viatu vya wazi, mwendo kasi na kubeba abiria zaidi ya mmoja na baadhi kubeba watoto wakati sheria hairuhusu.

Sheria ya usafirishaji wa Pikipikiya Sumatra hairuhusu mtoto wa chini ya miaka 8 haruhusiwi kupakiwa kwenye pikipiki bila msaada wa mtu mwingine.

Licha ya kampuni za kutengeneza helmeti kutengeneza kofia ngumu kwa watoto, lakini hapa nchini sheria imenyamaza kuhusu kofia ya mtoto aliyepanda na kusaidiwa na mzazi. Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani mkoani Morogoro, Boniface Mbao, anakiri kuwa kutovaa helmeti ni tatizo kubwa mkoani kwake.

Wanachofanya ni kuendelea kuwakamata madereva wakaidi lakini pia wanatoa elimu.

“Uelewa wa helmeti bado ni mdogo ndio maana tumekuwa tunafanya operesheni kubwa na tunapowakamata mbali l ya kuwalipisha faini, tunawaelimisha umuhimu wa kuvaa helmeti na faida zake,” anasema Kamanda Mbao.

Chanzo: Habari Leo

Sambaza Makala hii: Share on Facebook2Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn0Share on Google+0Email this to someone

You may also like

0 comments

By